Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA inasema, hifadhi ya raia Kivu Kaskazini ndio jukumu muhimu kabisa kwa sasa

OCHA inasema, hifadhi ya raia Kivu Kaskazini ndio jukumu muhimu kabisa kwa sasa

Msemaji wa Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA), Elizabeth Byrs, aliwaambia waandishi habari Geneva, leo hii, kwamba hali ya usalama katika Kivu, Majimbo ya Oriental na Equateur katika JKK, bado inaendelea kuwa mbaya zaidi.

Huduma za kuhifadhi raia waliopo katika Kivu Kaskazini ni kadhia iliopewa umuhimu wa hadhi ya juu kabisa, hasa baada ya kupokewa ripoti zinazoeleza makundi yenye kuchukua silaha yanaendelea kushiriki kwenye jinai ya kuiba mali za wanavijiji na kuangamiza mazao, na kwa wakati huo huo baadhi ya wafuasi wa magengi haya wameanza kuwakata viungo wakazi kadha wa vijijini. Kadhalika, kufuatia machafuko na mapigano yaliozuka baina ya makundi yanayohasimiana, kwenye sehemu za Baraka na Fizi, katika Kivu Kusini, baadhi ya mashirika ya kimataifa yasio ya kiserekali yamelazimika kuhamisha wafanyakazi wao na kuwapeleka eneo la Uvira kupata hifadhi. Vile vile, tume maalumu iliofanya makadirio kuhusu hali ya usalama kwenye maeneo ya Uvira/Baraka/Misisi imeinasihi UM kusitisha kwa muda, operesheni zake za kuhudumia kihali umma waathirika kwenye maeneo hayo, mpaka pale hali ya usalama itakapotengenea. Uamuzi huu utaathiri zaidi umma ulio dhaifu kihali unaoishi kwenye maeneo yaliovamiwa na uhasama, ambayo kikawaida hutegemea kufadhiliwa misaada ya kiutu na mashirika ya kimataifa. Katika Jimbo la Equateur, watu 22,000 wanaripotiwa walihama makazi na hivi sasa wamelekea taifa jirani la Jamhuri ya Kongo kuomba hifadhi. Halkadhalika, kwenye Jimbo la Oriental, mashambulio na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya raia ni mambo yaliosababisha maelfu ya raia kung'olewa makazi. Kwa mujibu wa taarifa za OCHA watu 456,000 waling'olewa makazi kwenye Jimbo hili kwa sasa.