Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa kimataifa wameakhirisha jukumu la kukamilisha itifaki ya Copenhagen juu ya mabadiliko ya hali ya hewa

Viongozi wa kimataifa wameakhirisha jukumu la kukamilisha itifaki ya Copenhagen juu ya mabadiliko ya hali ya hewa

Imeripotiwa hii leo kwamba viongozi wa kimataifa wameafikiana kuakhirisha yale majadiliano ya kufikia mapatano juu ya mabadiliko ya hali ya hewa katika mkutano ujao utakaofanyika mwezi Disemba katika Copenhagen, na badala yake wamekubaliana kwamba mkutano huu wa mabadiliko ya hali ya hewa ujaribu kufikia itifaki isio na uzito "wenye masharti ya kisiasa" ili kuwawezesha wajumbe wa kimataifa kuhakikisha masuala magumu yenye kutatanisha majadiliano yao yatazingatiwa kidhati katika siku za baadaye.

Mwelekeo huu kuhusu ajenda ya Mkutano wa Copenhagen uliidhinishwa Ijumapili kwenye mkusanyiko wa wajumbe wa kimataifa nchini Singapore. Ijapokuwa tangazo hili lilitafsiriwa na wengi kuwa linaashiria mazungumzo ya Copenhagen kutofanikiwa, na yatawasilisha mapatano yalio dhaifu kisheria, hata hivyo, Yvo de Boer, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya UM Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani (UNFCCC) alisema taarifa iliotolewa Singapore haimaanishi hata kidogo kuwa sasa hivi kumewekwa mipaka dhidi ya malengo ya kudhibiti taathira za mabadiliko ya hali ya hewa katika ulimwengu. Alisisitiza Mkutano wa Copenhagen wa mwezi Disemba utawajibika kufikia, kwa uwazi kabisa, makubaliano halisi ya kupunguza viwango vya utoaji wa hewa chafu katika anga ili kuanzisha vitendo vya pamoja, haraka iwezekanavyo, kudhibiti kipamoja madhara yanayoharibu mazingira kwa sababu ya hali ya hewa ya kigeugeu.