Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya KM inahimiza uharamia usitishwe Usomali na wakosa wafikishwe mahakamani

Ripoti ya KM inahimiza uharamia usitishwe Usomali na wakosa wafikishwe mahakamani

Ripoti mpya ya KM kuhusu hali ya uharamia na ujambazi katika mamlaka ya maeneo ya bahari ya mwambao wa Usomali, inayoambatana na Azimio 1846 la Baraza la Usalama, imechapishwa na kutolewa rasmi leo Ijumatatu, na imeeleza ya kuwa kuwepo kwa vyombo vya majeshi ya majini vya Mataifa Wanachama kwenye eneo hilo ni hatua muhimu iliosaidia kusawazisha utulivu wa mwambao wa Afrika Mashariki.

Lakini KM alihadharisha kwenye ripoti ya kuwa pia kunahitajika sera ilioungana, itakayojumlisha jitihadi za pamoja zitakazotumiwa kusawazisha hali kwenye maeneo ya katika bara nchini Usomali. Mwelekeo huu, lilisisitiza ripoti, unahitajia kuimarisha zaidi kazi za taasisi za usalama na sheria zitakazojazilisha mradi wa amani, na pia kuimarisha uwezo wa Serikali ya Mpito Usomali (TFG) pamoja na vikosi vya ulinzi amani vya UM kwa Usomali (AMISOM), kutenda shughuli zao vizuri zaidi kwenye ardhi ya Usomali. Kadhalika, ripoti ilipendekeza kufanyike uchunguzi maalumu, na kuwafungulia mashitaka, wale wote waliotuhumiwa kushiriki kwenye vitendo vya uharamia na ujambazi katika Usomali; na KM alipongeza tangazo la karibuni la Shirika la Polisi wa Kimataifa juu ya Makosa ya Jinai (INTERPOL) na Mataifa Wanachama la kuanzisha upelelezi kuhusu vyanzo vya asili vinavyofadhilia vitendo vya uharamia katika Usomali.