Skip to main content

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Baraza la Usalama lilikutana Ijumaa kwenye majadiliano ya hadhara ambapo, awali, lilisikia ripoti kutoka wenyekiti wa kamati tatu zinazohusika na utekelezaji wa mapendekezo ya Azimio 1267 juu ya masuala ya al-Qaeda na Taliban; Azimio 1373 dhidi ya vitendo vya ugaidi; na Azimio 1540, linaloambatana na masuala ya silaha za maangamaizi ya halaiki. Wenyekiti wa kamati hizi tatu ni mabalozi wa kudumu wa UM kutoka Austria, Croatia na Costa Rica ambao waliwasilisha taarifa kuhusu kazi za kamati zao katika miezi sita iliopita.

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti wahamiaji zaidi raia wanaendelea kuhajiri mastakimu, kutoka eneo la mapigano la Yemen kaskazini, kwenye jimbo la Sa'ada ambapo vikosi vya Serikali vinapambana na wapiganaji wa kundi la Al Houthi, mapambano ambayo yameingia mwezi wa nne hivi sasa. Wahamiaji hawa wanaomba hifadhi ya kujisitiri kwenye kambi za makazi ya muda na kwenye mastakimu ya familia za wenyeji wa maeneo jirani ya kusini. Wahamiaji wa ndani waliong'olewa makazi na mapigano, wenye kutafuta mahali pa kujisitiri huongeza shinikizo kwenye operesheni za UNHCR za kunusuru umma unaoteseka, na unaotegemea misaada ya kihali kutoka mashirika ya kimataifa. Mnamo siku chache zilizopita UNHCR inasema familia karibu 150 za wahamiaji zilisajiliwa kuwasili kwenye kambi za wahamiaji za Al Mazrak katika jimbo la Hajjah, takriban kila siku. Huu ni muongezeko wa aila 20 mpaka 30, zinazomiminikia kwenye eneo hilo kila siku kutafuta hifadhi. UNHCR imeripoti watu 10,000 sasa wanaishi kwa msongomano mkubwa kwenye kambi zilizofurika wahamiaji, na UNHCR imeripoti haina uwezo wa kuwahudumia mahitaji yao kama inavyotakiwa. Kwa mfano wahamiaji wamelazimika kuweka aila nne katika kila hema, ambalo limekusudiwa kuweka familio moja. UNHCR inajitahidi kuandaa hali itakayoridhisha mahitaji ya wahamiaji kwenye kambi inazohudumia, na inawasaidia watawala wenyeji kuharakisha ujenzi wa kambi mpya zitakazoweza kupokea wahamiaji elfu ziada ya raia wa Yemen waliong'olewa makazi kwa sababu ya mapigano. Tangu mwaka 2004, UNHCR inakadiria watu 175,000 waliathirika na mapiganao katika Yemen, ikijumlisha idadi ya wahamiaji wapya wanaoteseka na uhasama uliofumka nchini mwao katika miezi ya karibuni.

 Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu hii leo amekamilisha ziara ya wiki moja katika Brazil. Kwenye mahojiano na waandishi habari kufuatia ziara yake, alisema ijapokuwa Brazil ina kanuni za haki za binadamu za kuvutia kabisa kwenye madaftari ya sheria, na pia zimebuni sera kadha za kutia moyo kuhusu kanuni hizo, hata hivyo raia wenye jadi ya KiAfrika pamoja na wenyeji wa asili, bado wanaendelea kukabiliwa na ubaguzi wa rangi mbaya nchini mwao, pamoja na kukabiliwa na matatizo ya kutumiwa mabavu dhidi yao na vile vile kuteswa na udhalimu. Pillay alihadharisha ya kuwa bila ya makundi haya kukombolewa kutoka ufukara na hali duni, na kupatiwa huduma za kimsingi pamoja na fursa ya kupata ajira, yale maendeleo kadha mengineyo yalioshuhudiwa nchini yatazorota na hayatosarifika kwa masilahi ya wote.