Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA imeonya 'Hali Chad mashariki inahatarisha usalama wa wahudumia misaada ya kiutu'

OCHA imeonya 'Hali Chad mashariki inahatarisha usalama wa wahudumia misaada ya kiutu'

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti ya kuwa vitendo vya uharamia na ujambazi mbaya uliofanyika katika wiki mbili zilizopita, kwenye maeneo ya mashariki katika Chad, ni hali inayohatarisha operesheni za kiutu za kunusuru umma muhitaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya OCHA mfanyakazi wa kimataifa wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (ICRC) alitekwa nyara katika kipindi hicho, wakati mtumishi raia anayefanya kazi na shirika lisio la kiserikali linaloitwa Solidarité, aliuawa. OCHA ilisema mashirika matano, yasio ya kiserikali, pamoja na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu hivi sasa yamesitisha shughuli zao katika Chad mashariki. Hatua hii itaathiri hali ya watu 37,000 wanaotegemea kufarajiwa misaada ya kiutu na taasisi hizo. Ofisi ya OCHA, kwa sasa, ikijumlika na Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika Chad (MINURCAT) na serikali ya Chad kwa sasa wanajitahidi kuongeza shughuli za usalama, ili kuwalinda wafanyakazi wanaohudumia misaada ya kihali waliopo Chad. Mashirika yasio ya kiserikali 70 ziada yapo kwenye eneo la Chad mashariki ambayo sasa hivi yanahudumia misaada ya kiutu mbalimbali kwa wahamiajiwa kutoka Sudan na raia wazalendo walion'golewa makazi.