Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchanganyiko wa vitega uchumi na nia ya kisiasa huweza kufyeka njaa - FAO

Mchanganyiko wa vitega uchumi na nia ya kisiasa huweza kufyeka njaa - FAO

Ripoti mpya ya Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), iliochapishwa rasmi leo hii, yenye kutathminia maendeleo yaliofanyika kwenye nchi kadha inazozishughulikia, imebainisha kwamba idadi ya watu wasiopata chakula cha kutosha iliteremka kwa kiwango kikubwa, na cha kutia moyo.

Kwa mujibu wa fafanuzi za ripoti ya FAO, pakiwepo nia ya kisiasa miongoni mwa wabuni sera, ikichanganyika na uwekezaji maridhawa, hasa kwenye sekta ya kilimo, kutapatikana mafanikio ya kuridhisha katika kuhudumia chakula umma muhitaji. Ripoit iliangaza juu ya maendeleo yaliopatikana katika nchi 16, ambazo zimeshafanikiwa kufikia lile lengo la kupunguza, kwa nusu, idadi ya watu wenye njaa kwenye maeneo yao, kabla ya 2015, ili tarehe ya kukamilisha Malengo ya Maendeleo ya Milenia - ikijumlisha mataifa ya Armenia, Brazil, Nigeria na Vietnam. Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Jacques Diouf, leo ameanzisha kwenye mtandao wa intaneti, kampeni ya kupiga vita njaa duniani, kwa kutumia aina ya utaratibu wa teknolojia ya mawasiliano ya kisasa utakaokabidhiwa viongozi wa dunia watakaohudhuria Mkutano Mkuu juu ya Udhibiti Bora wa Akiba ya Chakula Duniani, utakaofanyika mjini Roma, Utaliana kuanzia tarehe 16 mpaka 18 Novemba, wiki ijayo.