Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM umeteua Julai 18 kuwa ni Siku Kuu ya Kimataifa Kumhishimu Nelson Mandela

UM umeteua Julai 18 kuwa ni Siku Kuu ya Kimataifa Kumhishimu Nelson Mandela

Ijumanne, kwenye kikao cha Baraza Kuu, kusailia mada muhimu inayohusu "utamaduni wa amani", Mataifa Wanachama yalipitisha, bila kupingwa, azimio la kuadhimisha tarehe 18 Julai, kila mwaka, kuwa ni ‘Siku ya Kimataifa Kumhishimu Nelson Mandela\'.

Tarehe hii ni siku aliyezaliwa mtetezi huyu shupavu, aliye mwanaharakati maarufu dhidi ya sera ovu za ubaguzi wa rangi katika Afrika Kusini. Azimio la Baraza Kuu limetambua uongozi adhimu, wa muda mrefu, wa Nelson Mandela katika kuleta umoja na kwenye harakati za ukombozi wa bara la Afrika. Kadhalika, azimio limetambua mchango mkubwa wa Mandela uliosaidia kuwasilisha Afrika Kusini huru, iliojikomboa na chuki za kikabila na ubaguzi wa kijinsia, taifa ambalo vile vile limewania kithabiti kufuata mfumo wa kidemokrasia na kuendeleza utamaduni wa amani kitaifa na kimataifa. ‘Siku Kuu ya Kimataifa Kumhishimu Nelson Mandela' itaanza kuadhimishwa rasmi na UM kuanzia mwaka 2010.