Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon siku ya leo anazuru Washington D.C. ambapo asubuhi alikutana na maofisa wa Makao Makuu ya Raisi wa Marekani (White House) wanaohusika na masuala ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni. Alasiri KM vile vile alikutana na viongozi wa Bunge la Marekani na walishauriana juu ya mada zinazofungamana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Katika taarifa iliotolewa alasiri na Ofisi ya Msemaji wa KM, ilieleza ya kuwa Ban Ki-moon amekaribisha tukio la kuundwa kwa serikali ya muungano wa taifa Lebanon. Alisema aliridhika ya kuwa, miezi mitano baada ya uchaguzi wa bunge kufanyika, mnamo tarehe 07 Juni 2009, viongozi wa makundi ya kisiasa katika Lebanon walifanikiwa kufikia mapatano ya kuridhisha na kuunda Baraza la Mawaziri. Aliongeza kusema ni matarajio yake viongozi wa kisiasa Lebanon wataendelea kufanya kazi kwa imani ya umoja, ushirikiano na kutumia utaratibu wa mazungumzo kutatua siotafahamu zao.

Asubuhi Baraza la Usalama lilizingatia suala la kuundwa kwa serikali Lebanon, kwa kuambatana na mapendekeezo ya azimio 1701. Mratibu Maalumu wa UM kwa Lebanon, Michael Williams, aliwasilisha ripoti mpya ya KM kuhusu utekelezaji wa azimio nambari 1701, ambalo ndani yake alielezea wasiwasi alionao kuhusu matokeo ya karibuni katika operesheni za Vikosi vya Muda vya UM katika Lebanon Kusini (UNIFIL). KM alishtumu ukiukaji wa aina yoyote wa azimio 1701, na alitoa mwito unaotaka kuwepo uangalifu wa kiwango cha juu juu ya usalama wa eneo la operesheni za vikosi vya UNIFIL. Kadhalika, Msaidizi KM juu ya Operesheni za Ulinziamani, Edmund Mulet aliwakilisha mbele ya Baraza la Usalama ripoti kuhusu shughuli za vikosi vya UNIFIL kwenye eneo la operesheni.

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM kwa Wahamiaji (UNHCR) ina wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa uhasama katika Yemen kaskazini na athari zake kwa raia. UNHCR imesihi juu ya umuhimu wa kuwapatia raia ulinzi unaofaa na kuhakikisha wahudumia misaada ya kiutu pia wanapata fursa ya kupeleka misaada ya kihali kwa umma muhitaji, bila pingamizi, na kuwahakikishia usalama, halkadhalika. Ripoti ya UNHCR inasema aila zilizon'golewa makazi kutoka eneo la mapigano katika jimbo la Sa'ada zinaendelea kuwasili kwenye kambi za makazi ya muda ya Al Mazrak, ambapo katika siku za karibuni kulishuhudiwa ongezeko kubwa la watu wanaowasili hapo, kujiepusha na mapigano. Mnamo mwisho wa wiki, katika Ijumamosi na Ijumapili, aila za wahamiaji 130/140 zimesajiliwa kuwasili kambini, na aila nyengine 80 ziliwasili Ijumatatu.

Ijumanne, kwenye mji wa Madrid, Uspeni, Helen Clark, Mkuu wa Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) akijumuika na Waziri wa Nchi wa Uspeni juu ya Ushirikiano wa Kimataifa, Soraya Rodriguez, walitia sahihi Maafikiano ya Ushirikiano kwa Miradi ya Maendeleo, kwa kipindi cha miaka mingi, mapatano ambayo yanagharamiwa kukaribia yuro milioni 400, fedha zitakazotumiwa kuimarisha ile miradi ya UNDP inayohusika na upunguzaji wa hali duni na kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye mataifa yanayoendelea. Mchango huu wa Uspeni, vile vile utatumiwa kufadhilia juhudi za kukamilisha Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) na kuendeleza utawala wa mfumo wa kidemokrasia, pamoja na kuzuia mizozo kufumka na katika kufufua shughuli za kiuchumi na jamii, ujenzi wa amani na pia kusaidia mageuzi katika UM yenyewe, na kwenye taasisi zake mbalimbali.