Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lengo la MDGs kupambana na UKIMWI linafanyiwa mapitio na UNAIDS

Lengo la MDGs kupambana na UKIMWI linafanyiwa mapitio na UNAIDS

Jumuiya ya Mashirika ya UM dhidi ya UKIMWI (UNAIDS), kwenye makala iliochapishwa wiki hii katika Jarida juu ya UKIMWI, imezingatia kwa makini zaidi, suala la kama jamii ya kimataifa itafanikiwa kuzuia maambukizi ya UKIMWI katika 2015, kwa kulingana na pendekezo rakamu ya sita ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs).

Makala ilikumbusha mataifa ya ulimwengu, kwa sasa, yamebakiza miaka mitano kabla ya 2015, na Jumuiya ya UNAIDS inajiuliza kama jamii ya kimataifa sasa hivi inao mfumo madhubuti, unaoridhisha, kupambana na janga la maambukizi ya VVU, na imetathminia pia maendeleo, kwa ujumla, katika kufikia lengo la kupunguza maambukizo mapya na kuzuia maradhi ya UKIMIWI duniani. Halkadhalika, UNAIDS imesailia, kwa kina, namna mataifa yanavyokusanya takwimu zao na kuripoti juu ya kutapakaa kwa VVU kwenye maeneo yao, na kama utaratibu huu unawiana na viwango vya kimataifa. Imeripotiwa ya kuwa uwiano wa nchi zilizowasilisha ripoti ya maendeleo kuhusu udhibiti wa maambukizi ya VVU, inaendelea kuongezeka kwa polepole na Mataifa Wanachama 150 yanasailiwa kuripoti juu ya kadhia hiyo, kwa hivi sasa.