Skip to main content

OCHA yaripoti watu 16,000 wang'olewa makazi Usomali na mafuriko

OCHA yaripoti watu 16,000 wang'olewa makazi Usomali na mafuriko

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti, kwa akali, watu 16,000 waling\'olewa makazi kwa sababu ya mafuriko katika majimbo ya Usomali ya Hiraan, Gedo na Shabelle ya Chini.

Wakati huo huo ugawaji wa chakula cha tiba, kilichopikwa tayari, kinachojulikana kama lishe ya Plumpy' Doz unatarajiwa kuendelea mwezi Novemba, kwenye maeneo yote ya Usomali ambapo mradi huo huwa unatekelezwa, yaani Usomali Kusini na Kati. Kadhalika, tangu mwezi Agosti, katika maeneo ya Afgooye na mji mkuu wa Mogadishu watoto 55,000, wenye umri wa baina ya miezi 06 mapaka 59, walifadhiliwa aina ya mchanganyiko wa chakula rutubishi kinachojulikana, kwa umaarufu, kama chakula cha UNIMIX. Mnamo wiki iliopita, Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), na Shirika la Afya Duniani (WHO) na washiriki wenzi, nao kwa upande wao vile vile walikamilisha kampeni ya kuhudumia afya raia wa Usomali wanaoishi katika wilaya ya Afgooye, kadhia iliokusudiwa kunusuru maisha ya watoto 54,000 chini ya umri wa miaka mitano pamoja na wanawake 62,000 wa umri wa kuweza kuzaa, pamoja na kuhudumia pia wale raia waliong'olewa makazi kwa sababu ya uhasama na mapigano.