Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon amesema ana matumaini serikali wanachama katika UM zitaweza kufikia mapatano juu ya masuala ya kimsingi, kwenye mkusanyiko wa Mkutano wa Copenhagen." Janos Pasztor, Mkurugenzi wa Tume ya KM Kushughulikia Masuala ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa amenakiliwa akisema ana imani mapatano anayoyazungumzia KM yatawakilisha "maudhui yenye sheria ya kuongoza utendaji wa kimataifa unaotakikana kudhibiti bora mabadiliko ya hali ya hewa katika dunia."

KM amenakiliwa akisema  'kuporomoka na kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, Ujerumani miaka ishirini nyuma, mnamo tarehe 09 Novemba 1989, ni kumbusho lenye kuthibitisha kihakika nguvu za mageuzi yanayoanzishwa na watu wa kawaida, kukidhi masilahi ya umma, kwa ujumla, nguvu zenye uwezo mkuu wa kutekeleza, kwa ufanisi zaidi, haki za binadamu na uhuru halali wa raia.  Kwa hivyo, KM aliyaomba Mataifa Wanachama kuwapongeza raia waliofanikiwa kuleta marekibisho ya Ujerumani miaka ishirini iliopita.

UM na mashirika wenzi yasio ya kiserikali, kwa mara nyengine tena wametoa mwito uitakayo Israel kuruhusu, haraka, kufunguliwa kwa vivuko vya kuingia Tarafa ya Ghaza na kuwawezesha WaFalastina kupata uwezo wa kupokea vifaa vya ujenzi vinavyohitajika kidharura kutengeneza majengo yalioharibiwa kwenye mashambulio ya mwanzo wa mwaka kwenye eneo, hasa ilivyokuwa majira ya mvua na baridi, ilisisitiza UM, yanakaribia kuanza. Mratibu wa Misaada ya Kiutu kwenye Maeneo Yaliokaliwa Kimabavu ya WaFalastina, Maxwell Gaylard, yeye kwa upande wake alikumbusha kwamba majira ya baridi yakiwasili "yatadhurui zaidi watoto wadogo wa Ghaza, ambao uvumilivu wao wa baridi kali na hali ya mvua mvua umeshadhoofishwa na ukosefu wa huduma za msingi na kuhanikiza kwa hali duni kwenye maeneo yao."

Ripoti iliochapishwa Ijumatatu na Shirika la Afya Duniani (WHO) juu ya matunzo ya afya ya wanawake duniani, imebainisha kidhahiri kwamba nchi nyingi bado zimeshindwa kukidhi kihakika mahitaji ya matunzo ya afya kwa wanawake katika kipindi muhimu cha maisha yao, mathalan, pale wanawake wanapotimia umri wa ujana au wanapofikia hali ya ukongwe. Ripoti ya WHO imekumbusha kwamba sasa hivi kunahitajiwa vitendo vya dharura kuendeleza afya na maisha ya wanawake, juu ya kuwa maendeleo kadha yalishuhudiwa duniani katika miongo ya karibuni, kwenye utekelezaji wa haki za kimsingi za wanawake, kwa ujumla.

Josette Sheeran, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani ameripotiwa kuukaribisha mwito wa karibuni uliotolewa na Warsha juu ya Mashirikiano ya Uchina na Afrika, wenye kuhimiza uwekezaji utakaodhibiti bora akiba ya chakula kwenye sekta za kilimo na miundombinu, ili kuhakikisha umma unapata chakula cha kutosha. Alisema kwa miaka mingi WFP imesaidia umma wa Uchina na Afrika kupata chakula kitakachowawezesha kuishi maisha yenye kuleta matunda na afya njema, baada ya kuwasaidia wakulima kulisha aila zao kwa kuimarisha ardhi za kulimia, na kujenga barabara, zahanati na maskuli kwa jamii husika.

Mnamo mwisho wa wiki iliopita, KM Ban Ki-moon alihudhuria mkutano juu ya Kampeni ya Vijana wa Dunia Kutumikia Dini Kupunguza Silaha na Kuimarisha Usalama uliofanyika Costa Rica. Ijumamosi, KM alihutubia wajumbe wa kimataifa ambapo aliwahimiza kuongeza bidii zao katika kuondosha silaha na kuziangamiza, na baadaye kuwekeza fedha zinazotumiwa kwenye silaha kuimarisha kadhia ya amani na ustawi wa uchumi na jamii. Alikumbusha, gharama ya fedha zinazotumiwa kila mwaka kutengeneza silaha duniani kwa sasa zimeshakiuka dola trilioni moja, na wakati huo huo misaada ya kuhudumia maendeleo ya uchumi na jamii imedididimia na kuteremka na kufikia kiwango cha chini kabisa, tukilinganisha na posho inayotumiwa kutengeneza silaha za kuangamiza. Alihadharisha, silaha zikiendelea kutengenezwa kimataifa kadhia hii "itafurika soko za dunia, na kuvuruga jamii kadha wa kadha ulimwenguni, na kawaida hupalilia cheche za moto zinazorutubisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na ugaidi katika sehemu mbalimbali za dunia" na ni lazima kukomeshwa kwa usalama na amani ya kimataifa.