Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM inahamisha na kuwatawanya wafanyakazi wake Afghanistan kuwapatia usalama unaoridhisha

UM inahamisha na kuwatawanya wafanyakazi wake Afghanistan kuwapatia usalama unaoridhisha

Shirika la UM la Kuisaidia Afghanistan Kurudisha Utulivu (UNAMA) Alkhamisi lilitangaza ya kuwa limeamua kuhamisha baadhi ya wafanyakazi wake, waliopo katika sehemu kadha wa kadha nchini Afghanistan, na kuwapeleka kwenye makazi ya muda ndani ya nchi, na wengine nje ya taifa hilo, kwa matarajio ya kuwapatia ulinzi unaofaa.

Hatua hii ilichukuliwa ili kuimarisha usalama wa wafanyakazi hawo wa UM, kufuatia mashambulio maututi yaliofanyika wiki iliopita, kwenye mji wa Kabul, ambapo watumishi watano wa UM waliuawa na wengineo tisa walijeruhiwa kwenye makazi yao. Kwa mujibu wa Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afghanistan, ambaye pia ni Mkuu wa Shirika la UNAMA, Kai Eide, kitendo hiki ni cha muda, na kisitafsiriwe hata kidogo kama UM, umesalimu amri na unasitisha shughuli zake katika Afghanistan.  Alisema, kwa sababu ya kujiri kwa hali ya dharura UNAMA mnamo wiki mbili iliopita, shirika limewajibika kuchukua hadhari inayotakikana kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wake katika kipindi hiki kigumu, na kwa wakati huo huo pia kuhakikisha operesheni za kuhudumia misaada ya kiutu katika Afghanistan zitaendelezwa kote nchini, na hazitopwelewa, kwa minajili ya masilahi ya umma.

Sikiliza  ripoti kamili kwenye idhaa ya mtandao.