Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ijumaa alasiri KM Ban Ki-moon alihutubia Baraza la Usalama, kwenye kikao maalumu cha faragha, kuzingatia hali katika Afghanistan. Alitazamiwa kusailia hali ya usalama na kuwasilisha fafanuzi zake juu ya ziara aliifanya majuzi kwenye mji wa Kabul, Afghanistan kufuatia shambulio la magaidi dhidi ya watumishi wa UM, tukio liliosababisha vifo vya wafanyakazi watano na majeruhi tisa.

Alkhamisi jioni, Baraza Kuu la UM limepitisha azimio la kuidhinisha ripoti ya tume ya uchunguzi kuhusu ugomvi uliosababisha mashambulio yaliotukia mwanzo wa mwaka, dhidi ya eneo liliokaliwa la Tarafa ya Ghaza, ripoti ambayo iliwatia hatiani vikosi vya jeshi la Israel pamoja na wapiganaji wa KiFalastina, kwa makosa ya kukiuka pakubwa haki za binadamu dhidi ya raia. Baada ya majadiliano ya siku mbili, katika Makao Makuu ya UM yaliopo kwenye jiji la New York, Mataifa Wanachama 114 yalipiga kura ya kuunga mkono azimio linaloidhinisha matokeo ya uchunguzi wa tume na yale mapendekezo ya kuchukua hatua ziada juu ya suala hili. Mataifa 18 yalipiga kura ya kupinga azimio, wakati nchi 44 nyengine kutopiga kura. Uchunguzi juu ya ukiukaji wa haki za binadamu uliotukia wakati wa mashambulio ya Ghaza, uliongozwa na Jaji Richard Goldstone wa Afrika Kusini, aliyekuwa mwendesha mashitaka wa mahakama za UM juu ya makosa ya jinai ya vita katika Rwanda na Yugoslavia ya zamani. Ripoti ilisema makundi yote mawili - yaani jeshi la Israel na wapiganaji wa KiFalastina - walipatikana na hatia ya kuharamisha kanuni za kimataifa za kiutu, hali ambayo ilifananishwa na makosa ya jinai dhidi ya ubinadamu, yalioendelezwa mnamo kipindi cha baina ya Disemba 2008 hadi Januari 2009. Baada ya azimio kupitishwa, Raisi wa Baraza Kuu Ali Treki aliwaambia waandishi habari waliopo Makao Makuu kwamba "kura iliopitishwa ilijumuisha mwito muhimu katika sheria ya kimataifa, inayopinga dhahiri ile tabia ya kutenda makosa dhidi ya sheria bila kujali adhabu" mwito ambao alisema ulitetea "haki na uwajibikaji wa wakosa kwa matendo yao." Aliongeza kusema kwa kusisitiza ya kuwa "bila haki kutekelezewa waathirika husika, maendeleo ya amani yatawapiga chenga umma wa kimataifa." Raisi wa Baraza Kuu alikumbusha tena kwamba "utu wa mwanadamu ni lazima uhishimiwe, na kutambua haki halali alizojaaliwa nazo kimaumbile, bila kujali dini, uraia wala kabila."

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti, kwa akali, watu 16,000 waling'olewa makazi kwasababu ya mafuriko katika majimbo ya Usomali ya Hiraan, Gedo na Shabelle ya Chini. Wakati huo huo ugawaji wa chakula cha tiba, kilichopikwa tayari, kinachojulikana kama lishe ya Plumpy' Doz unatarajiwa kuendelea mwezi Novemba, kwenye maeneo yote ya Usomali ambapo mradi huo huwa unatekelezwa, yaani Usomali Kusini na Kati. Kadhalika, tangu mwezi Agosti, katika maeneo ya Afgooye na mji mkuu wa Mogadishu watoto 55,000, wenye umri wa baina ya miezi 06 mapaka 59, walifadhiliwa aina ya mchanganyiko wa chakula rutubishi kinachojulikana, kwa umaarufu, kama chakula cha UNIMIX. Mnamo wiki iliopita, Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), na Shirika la Afya Duniani (WHO) na washiriki wenzi, nao kwa upande wao vile vile walikamilisha kampeni ya kuhudumia afya raia wa Usomali wanaoishi katika wilaya ya Afgooye, kadhia iliokusudiwa kunusuru maisha ya watoto 54,000 chini ya umri wa miaka mitano pamoja na wanawake 62,000 wa umri wa kuweza kuzaa, pamoja na kuhudumia pia wale raia waliong'olewa makazi kwa sababu ya uhasama na mapigano.

Ray Chambers, Mjumbe Maalumu wa KM KKudhibiti Malaria, ameripotiwa kupongeza mchango wa UNICEF ambapo msaada wa dola milioni 8.5 ulitengwa makhsusi kuhudumia ugawaji wa vyandarua vilivyonyunyiziwa dawa ya kuua vijidudu, katika mataifa ya Afrika yaliopo kusini ya Sahara. Chambers alisema mchango huu utasaidia kunusuru maisha ya watoto wachanga milioni 40 dhidi ya maambukizi ya maradhi maututi ya malaria. Vyandarua milioni 150 vilivyotiwa dawa ya kuua vijidudu vinavyoambukiza malaria vitapelekwa kwenye mataifa hayo ya Afrika katika mwaka ujao.