Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Leo Alkhamisi KM Ban Ki-moon yupo njiani akirejea New York, baada ya kukamilisha ziara ya Ugiriki. Kabla ya kuondoka Ugiriki asubuhi alihutubia Bunge la Helleniki, na kuwa KM wa kwanza kihistoria kufanya hivyo. Aliwaambia wabunge wa Ugiriki kwamba ziara aliofanya Kabul, mapema wiki hii, ilimtia hamasa sana baada ya kushuhudia ushupavu na dhamana walionyesha watumishi wa UM, wanaohatarisha maisha, kuhudumia umma wa Afghanistan, na alisisitiza kazi muhimu za UM nchini humo hazitopwelewa kwa sababu ya mashambulio ya karibuni, na aliahidi zitaendelea kutekelezwa licha ya kuwepo hatari kadha wa kadha dhidi ya watumishi wa kimataifa. Vile vile KM alizungumzia kuhusu matarajio yake juu ya maafikiano kwenye majajdiliano yaudhibiti bora wa mabadiliko ya hali ya hewa. Alikumbusha majadiliano ya Copenhagen ni mazito na magumu kwa sababu hujumuisha watendaji wengi na maafikiano ya vipande vipande; na ailitilia mkazo ni muhimu kwa Mataifa Wanachama kuwa na makubaliano ya pamoja, yalio ya jumla, yenye wizani wa kuridhisha, pamoja na usawa na hukumu ya lazima.

Taarifa ya karibuni ya Idara ya Kuhudumia Shughuli za Nje za Operesheni za Amani za UM (DFS), imeripoti kwamba kuanzia mwezi Januari 2009, Mataifa Wanchama yaliochangisha vikosi vyao na UM kulinda amani kimataifa, yameripoti kutoa adhabu kwa jumla ya wanajeshi 33 waliokutikana na makosa ya udhalilishaji wa kijinsia na jinai ya kujamii kimabavu wakati wakiendeleza huduma zao katika mataifa ya nje. Adhabu hizi zinajumlisha wanajeshi kufukuzwa jeshini, kulazimishwa kustaafu, kunyanganywa vyeo vya uofisa, na wengine walihukumiwa vifungo vya muda mrefu nchini mwao. Mwaka jana wanajeshi walinzi amani wawili walipewa adhabu kama hizo, na katika 2007 wanajeshi 15 walihukumiwa kukiuka kanuni za kimaadili za UM wakati wanashiriki kwenye shughuli za kulinda amani. Halkadhalika, katika miaka mitatu iliopita wanajeshi ishirini waliofanya makosa kinyume na kanuni za operesheni za amani za UM, walihukumiwa adhabu, mathalan, kwa kupoteza silaha, makosa ya kukiuka kanuni za usalama wa barabarani, vitendo vya ulaghai na wizi. Kesi za kukiuka nidhamu za ulinzi amani za UM ziliwahusu wanajeshi walioshiriki kwenye operesheni zinazoendelezwa katika mataifa ya JKK, Haiti, Lebanon, Cote d'Ivoire, Liberia na Sudan.

Asubuhi kuliitishwa kikao cha hadhara kwenye Baraza la Usalama kufuatia mashauriano kuhusu hali katika Guinea-Bissau. Joseph Mutaboba, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Guinea-Bissau, aliwaambia wajumbe wa Baraza la Usalama kwamba Serikali ya taifa analolishughulikia inajitahidi kudhibiti athari za mauaji ya watu mashuhuri yaliotukia nchini humo katika miezi ya Machi na Juni 2009. Alisema kuna utambuzi kwamba maendeleo machache yalipatikana kwenye zile sekta muhimu za utawala. Alitilia mkazo ni lazima kwa wenye madaraka kuhakikisha tabia ya kufanya makosa bila kujali adhabu ikomeshwe nchini haraka. Vile vile alinasihi kwamba ni muhimu kwa watawala kufufua imani ya raia juu ya uhalali wa mifumo ya sheria, kitendo ambacho kikitekelezwa kama inavyotakikana kitachangisha katika kurudisha upatanishi wamakundi ynayohasimiana ndani ya nchi. Kadhalika, Antonio Maria Costa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya UM juu ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC) alizungumzia kikao cha Baraza la Usalama juu ya Guinea-Bissau. Alieleza kwenye risala yake ya kuwa katika miezi 18 iliopita, kulishuhudiwa miporomoko mikubwa katika ukamataji wa madawa ya kulevya katika eneo la Afrika Magharibi. Hata hivyo, alionya ya kuwa ukanda wa Afrika Magharibi hivi sasa unaonekana unanyemelea kutambuliwa kama ndio chanzo cha madawa ya kulevya kieneo, na sio mahali pa kupitishia bidhaa hizo haramu.

Naibu KM (NKM) Asha-Rose Migiro yupo Addis Ababa kwa sasa. Anaripotiwa leo kuhutubia Kikao cha 10 cha UM juu ya Utaratibu wa Kikanda Kuratibu Maendeleo. Alisema juhudi za katika bara la Afrika kutekeleza, kwa wakati, Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs), zimo hatarini kutokana na athari haribifu za mizozo ya kiuchumi duniani, kwa sababu maendeleo ya mataifa ya Afrika hutegemea zaidi biashara ya kuuza bidhaa zao nje. Alihadharisha "licha ya kuwepo mafanikio fulani yanayotambulika, kusema kweli, maendeleo ya MDGs, kwa ujumla, barani Afrika hayapo kwenye mkondo unaoridhisha", na linalosumbua zaidi, alitilia mkazo, ni ukosefu wa maendeleo katika huduma za kuimarisha afya ya uzazi. Aliyasihi mataifa yaliohudhuria mkutano kutekeleza mapendekezo ya Kundi la Uongozi juu ya Utendaji wa Malengo ya MDGs.