Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalamu huru wa UM aihimiza Mauritania kuongeza bidii ya kufyeka milele utumwa mamboleo

Mtaalamu huru wa UM aihimiza Mauritania kuongeza bidii ya kufyeka milele utumwa mamboleo

UM umeripoti kwamba Serikali ya Mauritania na jumuiya za kiraia zimeshirikiana kuchukua hatua muhimu, ili kupambana na aina mpya ya utumwa mamboleo katika nchi.

Wameamua kuwakilisha mkabala wa jumla, utakaotumiwa kupambana na tatizo hili, kwa ushirikiano wenye uwezo unaosarifika, kwa kuzingatia aina zote za ubaguzi pamoja na umaskini uliopamba kwenye matabaka yote ya kijamii. Gulnara Shahinian, Mtetezi wa UM dhidi ya utumwa mamboleo, baada ya kuzuru Mauritania majuzi, alisema alishuhudia maendeleo, kwenye juhudi za Serikali za kukomesha janga hili la kijamii; lakini vile vile, alitilia mkazo, kwamba kunahitajika kuwepo miradi rasmi ya jumla itakayotumiwa kufyeka milele suala la utumwa mamboleo nchini humo. Alionya, mifumo yote ya utumishi usiolipwa chochote katika karne ya sasa, mathalan, ujakazi na utumwa mamboleo, ni vitendo vinavyohitajia kukomeshwa haraka maana husababisha vizingiti kubwa dhidi ya "utulivu, maendeleo yanayosarifika na ustawi wa taifa". Mtetezi wa haki za binadamu wa UM alipongeza Mauriatnia, kwa kuchukua hatua za kisheria kufyeka utumwa mamboleo, hasa ile sheria iliopitishwa 2007, ilioharamisha aina zote za utumwa katika nchi.