Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo muhimu yamepatikana Sudan Kusini katika upokonyaji wa silaha

Maendeleo muhimu yamepatikana Sudan Kusini katika upokonyaji wa silaha

Mjumbe Maalumu wa UM kwa Sudan, Ashraf Jehangir Qazi, Ijumanne, kwenye mazungumzo ya duru ya meza nchini Sudan juu ya taratibu za kuwajumuisha kwenye maisha ya kawaida wapiganaji wa zamani, alipongeza mafanikio yaliopatikana mwaka huu kwenye utekelezaji wa mradi wa kupokonya, kutawanya na kuwaunganisha na maisha ya kijamii wale wapiganaji wa zamani wanaokadiriwa 15,000, walioshiriki kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ya miaka mingi kati ya Sudan Kaskazini na Sudan Kusini.

Mradi unaojulikana kama mpango wa DDR, ulioanzsihwa mwezi Februari 2009, unatarajiwa kuwaunganisha waliokuwa wapiganaji, na maisha ya kawaida, kwa kuambatana na Mapatano ya Jumla ya Amani (CPA), yaliosaidia kusimamisha mapigano ya miaka mingi katika Sudan. Qazi alisema mradi wa DDR "umewapa matumaini waliokuwa wapiganaji, pamoja na jamii zao, ya kupata maisha bora, baada ya kushuhudia hatua halisi zinachukuliwa kitaifa kuendeleza amani." Vile vile Qazi alieleza UM, sasa hivi, unajumuika na mashirika wenzi katika Sudan kupanua miradi ya kupokonya silaha katika maeneo mbalimbali ya nchi. Kadhalika, Qazi, ambaye pia ni mkuu wa Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani Sudan Kusini (UNMIS), alikumbusha ya kuwa hatua ya kuwajumuisha waliokuwa wapiganaji na maisha ya kikawaida, hasa wale wapiganaji wa makundi ya waasi ya SAF na SPLA, ilikuwa ni "fursa muhimu katika kuandaa mazingira yanayoaminika yatakayoasaidia kuendeleza, kwa amani, uchaguzi ujao wa taifa." Halkadhalika, Qazi alihadharisha kwamba kuna upungufu mkubwa wa fedha zinazohitajiwa na Shirika la UNICEF, kuwahudumia wapiganaji watoto na kuwajumuisha kwenye maisha ya kawaida, na inakhofiwa pindi msaada huu utaendelea kuzorota, kuna hatari watoto hawa huenda wakarejea kwenye kambi za wapiganaji na kuchochea vurugu kwa mara nyengine tena.