Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Kwenye taarifa aliotoa KM Ban Ki-moon Ijumanne, kwa waandishi habari, alielezea kuvunjika moyo juu ya kuendelea kwa vitendo visio halali vya Israel, kwenye eneo liliokaliwa kimabavu la Jerusalem Mashariki, ambapo alisema nyumba za WaFalastina zilibomolewa kihorera, na aila kadha zilifukuzwa kutoka majumbani mwao, mastakimu ambayo baadaye walikabidhiwa walowezi wa Kiisraili waliojisakama, kwa nguvu, katika mitaa ya WaFalastina. Vitendo hivi, alionya KM, ni miongoni mwa mambo yenye kupalilia mazingira ya wasiwasi na kudhoofisha zaidi hali ya kuaminiana miongoni mwa makundi yanayohusika na mvutano wa Mashariki ya Kati. Aliisihi Israel kusitisha, halan, vitendo hivi vya uchokozi. Kadhalika, KM alitoa mwito ziada unaoitaka Israel kutekeleza zile ahadi ilizotoa kabla, kuhusu mapendekezo ya Ramani ya Amani juu ya Suala la Mashariki ya Kati, na kusimamisha shughuli zake zote kwenye makazi ya walowezi, ikijumlisha pia vile vitendo vya kutaka kupanua zaidi majengo yaliopo kwenye maeneo yaliokaliwa; na vile vile Israel ilinasihiwa ing\'oe haraka vituo vyote vya mbali vya uangalizi na, hatimaye, iruhusu taasisi za KiFalastina zifunguliwe baada ya kufungwa kwa kitambo, ili zianze kuendesha shughuli zake halali katika eneo la Jerusalem Mashariki.

Naibu KM(NKM) Asha-Rose Migiro aliripotiwa kuwasili Addis Ababa, Ethiopia siku ya leo kutokea Beirut, Lebanon ambapo Ijumanne alikutana na Raisi Michel Sleiman, na vile vile alionana na waratibu wa miradi ya maendeleo ya kikanda ya UM. Kadhalika NKM alipokuwepo Beirut alihutubia mkutano uliozingatia Mfumo wa Kuratibu Hali ya Dharura ya Kikanda. Kwenye risala yake NKM alisema UM sasa hivi unajiandaa kuanzisha Mfumo wa Dunia Kuhadharisha Uwezekano wa Kuathiriwa kidharura, utaratibu utakaozipatia nchi husika, kwa wakati, takwimu halisi na fafanuzi zinazofaa kuhusu huduma kinga za watu maskini na walio dhaifu ambao huenda wakadhuriwa na mizozo ya kikanda. NKM aliziomba serikali za eneo kushirikiana na UM ili kuhakikisha kutakuwepo mfumo wa kutoa hadhari za mapema, unaofaa, na ulio madhubuti. Halkadhalika, NKM Asha-Rose Migiro aliwasihi maofisa wa kienyeji na wale wa kutoka UM kuendelea kujihusisha na juhudi za mataifa ya Mashariki ya Kati za kukidhi, kwa wakati, Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs), ambayo huebda yakapuuzwa na mchango haba pindi patazuka mizozo isotarajiwa.

Mnamo Ijumatano ya leo, kutokea Geneva, UM umewasilisha sera mpya itakayotumiwa kumudu ajira inayoweza kusarifika, kufuatia kusimamishwa kwa mapigano na vurugu kwenye nchi zilizoshuhudia mapigano na uhasama. Mpango huu wa UM unajulikana kama Sera ya Kuunganisha na Kuzalisha Ajira na Mapato Kufuatia Migogoro, na imekusudiwa hasa kuchangisha amani ya kudumu kwenye mazingira yaliojaa kigeugeu, kwa kuwapatia raia ajira yenye pato zuri na linaloweza kutegemewa. Sera ilibuniwa baada ya kufanyika mashauriano ya miaka mitatu, yalioongozwa na Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) na Shirika la Haki za Wafanyakazi (ILO). Sera inatazamiwa kutekelezwa, awali, kwenye zile nchi tano zilizoibuka kutoka hali ya uhasama na mapigano katika miaka ya karibuni: ikijumlisha Burundi, Côte d'Uvoire, Nepal, Sierra Leone na Timor-Leste.