KM ana matumaini juu ya matokeo ya Mkutano wa Copenhagen

KM ana matumaini juu ya matokeo ya Mkutano wa Copenhagen

KM Ban Ki-moon, alinakiliwa akisema anaamini itifaki muhimu itakamilishwa mwezi ujao, kwenye Mkutano Mkuu wa Copenhagen, kuhusu udhibiti bora wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

Alihadharisha mapatano hayo hayatomaanisha kuwa kauli ya mwisho ya makubaliano, juu ya kanuni mpya za kupunguza hewa chafu inayoharibu mazingira, sheria ambazo zinatarajiwa kuurithi Mkataba wa Kyoto. KM alisema penye nia ya kisiasa bila ya shaka patakuwepo pia njia itakayoleta suluhu ya kuridhisha kwa wote, na alitumai kikao kijacho cha Copenhagen kitawasilisha maafikiano muhimu ya kihistroia. KM aliyasema hayo baada ya chai ya asubuhi iliojumuisha majadiliano ya kazi na Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, tukio liliofanyika Ijumanne mjini London. KM alisema yeye na Gordon Brown wamekubaliana kuwa watafanya kila wawezalo, kuhakikisha mkutano wa Copenhagen wa mwezi ujazo utakamilishwa kwa mafanikio yatakayoridhisha fungu kubwa la Mataifa Wanachama.