Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yapeleka misaada ya dharura kufarajia Waangola waliofukuzwa JKK

UNHCR yapeleka misaada ya dharura kufarajia Waangola waliofukuzwa JKK

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limetangaza kuwa Ijumamosi, ilituma Angola, kutoka Afrika Kusini, ndege zilizobeba shehena ya misaada ya kufarajia kihali, makumi elfu ya raia wa Angola waliorejea nchini kwao mwezi uliopita, baada ya kufukuzwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK).

Ndege ya aina ya Boeing 747 iliwasili Luanda, mji mkuu wa Angola, katika saa za magharibi na mahema 2,250 pamoja na mikeka ya kulalia 5,000, na mablanketi 4,000, na vile vile maghala ya muda yaliokwisha jengwa viwandani. Vifaa vyote hivi vilisafirishwa kutokea ghala za UNHCR za Durban zilizorimbikiza misaada ya kukidhi mahitaji ya dharura, baada ya kupokea maombi kutoka Serikali ya Angola juu ya msaada huo. Baada ya misaada ya dharura kuwasili Luanda, ilihamishwa kwenye mdege za kijeshi na kupelekwa kwenye majimbo ya Uige na Zaire, Angola kaskazini, yaliopakana na JKK. Kwa mujibu wa Serikali ya Angola, idadi ya raia wa Angola waliofukuzwa kutoka JKK, ikijumuika na wale waliorejea kwa khiyari, wanaohitajia misaada ya kimataifa kumudu maisha inajumlisha watu 50,000; na asilimia kubwa yao walisajiliwa kama wahamiaji wa dharura katika JKK; lakini walinyimiwa fursa ya kuchukua hata mali na vikorokoro vyao pale walipolazimishwa kuihama JKK na kurejeshwa makwao kimabavu.