Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Michele Montas, Msemaji wa KM aliulizwa kwenye mahojiano ya Ijumanne na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu kama kuna ukweli juu ya madai ya ripoti ya shirika lisio la kiserikali, linalochunguza utekelezaji wa haki za binadamu linaloitwa Human Rights Watch, kuhusu ukiukaji wa haki za kiutu uliofanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mwaka huu, ambapo wanajeshi wa brigedi ya 213 ya Vikosi vya Taifa vya FARDC walituhumiwa kushiriki kwenye “mauaji na uvunjaji sheria dhidi ya darzeni ya raia” katika eneo la mashariki la JKK. Alain Le Roy, Naibu KM juu ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM, anayezuru eneo la mashariki la JKK, mapema wiki hii, alinakiliwa akisema Ijumatatu kwamba Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) na jeshi la FARDC wanalazimika kuanzisha, haraka, uchunguzi juu ya madai ya ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya raia ulioendelezwa na wanajeshi wa taifa; na wakati huo huo alitangaza MONUC itasitisha mchango wake kwenye uenezaji na usafirishaji wa wanajeshi wa brigedi 213 ya FARDC kwenye operesheni za pamoja, ili kusubiri matokeo ya uchunguzi juu ya wanajeshi waliohusika na vitendo haramu dhdi ya raia vilivyofanyika katika eneo la mashariki la JKK. Msemaji wa KM Michele Montas aliwaambia waandishi habari wa Makao Makuu, New York kuna “ushahidi unaoaminika” kwamba wanajeshi wa FARDC walihusika na mauaji ya raia 62, ikijumlisha fungu kubwa la wanawake na watoto wadogo, yaliofanyika katika eneo la mapigano la Lukweti, kwenye jimbo la Kivu Kaskazini, baina ya miezi ya Mei na Septemba 2009. Vikosi vya MONUC katika siku za nyuma vilishirikiana na wanajeshi wa FARDC kwenye operesheni za kuwang’oa waasi Wahutu wa Rwanda waliopiga kambi katika Kivu Kaskazini.

Ripoti mpya ya Shirika la UM juu ya Haki za Wafanyakazi (ILO) imethibitisha, kwa mwaka wa pili mfululizo kwamba mishahara katika dunia inaendelea kuporomoka. Ripoti ya 2009 yenye kichwa kisemacho "Ripoti juu ya Mishahara Kimataifa" imeonyesha uongezaji wa kima cha mishahara ni kadhia iliopwelewa kwa kiwango kikubwa katika 2008 kwa sababu ya kuzuka kwa mizozo ya kiuchumi katika wakati huo, na kiwango hicho kinatarajiwa kuanguka zaidi katika mwaka huu. Taarifa ya ILO pia ilisema hali hii inatilia mashaka juu ya yale madai ya kufufuka kwa kadhia za kiuchumi kijumla katika masoko ya kimataifa.

Sha Zukang, Naibu KM wa UM juu ya Masuala ya Kiuchumi na Jamii, yupo mjini Washington D.C. hii leo akishiriki kwenye Mkutano Mkuu wa Dunia, wa siku tatu, juu ya Bunge la Teknolojia ya Mawasiliano ya Kisasa. Mkutano uliotayarishwa na Idara ya UM juu ya Masuala ya Uchumi na Maendeleo (ECOSOC), Bunge la Wawakilishi Marekani na pia Jumuiya ya Mabunge ya Kimataifa, utasailia taratibu zinzofaa kutumiwa na Teknolojia ya Mawasiliano ya Kisasa na Habari (ICT) ili kuimarisha majukumu ya mabunge kutawala vyema na kuhakikisha mfumo wa kidemokrasia unashika mizizi inayotakiwa pamoja na kukuza maendeleo. Kwenye hotuba ya ufunguzi, Sha Zukang alisema kwamba, licha ya uwezo dhahiri uliojiri wa teknolojia ya ICT, na juu ya maendeleo yaliopatikana kuhusu uwezo wa kutumia utamaduni wa mawasiliano ya kisasa, bado kuna pengo kubwa kuhusu matumizi ya teknolojia ya mawasilianoya kisasa baina ya nchi zenye maendeleo ya viwanda na mataifa yanayoendelea.