Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa wanachama 187 yalaumu vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba kwenye Baraza Kuu

Mataifa wanachama 187 yalaumu vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba kwenye Baraza Kuu

Mnamo Ijumatano ya wiki hii, kwa mwaka wa 18 mfululizo, wawakilishi wa kimataifa kwenye Baraza Kuu la UM walipiga kura ya kuunga mkono, kwa mara nyengine tena, azimio la kuishtumu Marekani kwa vikwazo vyake vya kiuchumi, kifedha na kibiashara dhdi ya Cuba.

Kura ya mwaka huu ya Baraza Kuu juu ya suala hili iliyahamasisha Mataifa Wanachama 187, kati ya nchi 192, kutia kura ya upendeleo, kulaumu vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba. Mataifa ya Marekani, Israel na Palau ndio nchi tatu pekee zilizotia kura ya kupinga azimio, wakati Mataifa ya Visiwa vya Marshall na Micronesia kuamua kutotia kura zao.

Vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Cuba, ambavyo vinatafsiriwa kama ni mazingio ya kiuchumi, kwa namna taathira zake zinavyodhuru na kutishia kimataifa, ni vizuizi vilivyoekewa Cuba na Marekani takriban nusu karne. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Cuba, Bruno Rodriguez Parrilla, alipohotubia majadiliano kuhusu suala hili alikumbusha licha ya kuwa kuna mregezo kidogo juu ya uhusiano baina ya Marekani na Cuba sasa hivi, hata hivyo, chini ya utawala wa serikali ya sasa ya Marekani vikwazo hivyo dhidi ya Cuba vinaendelezwa bado. Alielezea ni matatizo ya aina gani huikabili Cuba kutokana na vikwazo au tuseme mazingio ya kiuchumi dhidi ya taifa lake:

"Inasababisha upungufu mubwa wa vitu. Inazorotisha uwezo

wetu halisi wa kukuza maendeleo, na hutuharibia vibaya sana huduma zetu za kiuchumi. Bila ya shaka yoyote, kimsingi, vikwazo vya Marekani ndivyo vinavyokwamisha maendeleo hakika ya uchumi wa nchi yetu. Tathmini ya hali ya juu, na takwimu za kihafidhina, zimethibitisha wazi, na kihakika, hasara kuu iliopata Cuba kiuchumi, ambayo inagharamiwa kufikia mamia bilioni ya madola, hasa tukifungamanisha hesabu hizo na miporomoko ya thamani ya dola ya Kimarekani katika soko la kimataifa."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba alisisitiza, mazingio ya kiuchumi ya Marekani dhidi ya Cuba, hayajakusudiwa kuadhibu na kuitesa Cuba tu, bali pia yamedhamiria kuzuia hata nchi nyengine huru, wanachama wa UM, zisifanye biasahara na Cuba. Akizungumza kwa niaba ya mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, Balozi wa Sweden katika UM, Anders Liden alishtumu vikwazo vya uchumi vya Marekani, ambavyo alisema anaamini vimekiuka mipaka ya sheria za kimamlaka, kwa kushurutisha mataifa nje ya Marekani kutekeleza vikwazo hivyo:

"Sheria za Marekani, mathalan, ile Sheria ya 1992 juu ya Demokrasia kwa Cuba na pia Sheria ya Helms-Burton ya 1996, ni kanuni zilizojaribu kukuza na kupanua madaraka ya sheria ya Kimarekani kwa nchi ziliopo nje ya mamlaka yake. Kwa kuambatana na kanuni na maadili ya wanachama wa mataifa wa Umoja wa Ulaya, nchi hizi zinakataa, na zitaendelea kupinga, kidhati, uingiliaji kati wa uhuru wa mamlaka yao kwa kutaka kulazimisha kufuata sheria za nchi za kigeni, kinyume na maadili wanayofuata juu ya uhusiano wa kimataifa."

Lakini juu ya kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) yalitia kura ya kulaani vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba, Balozi wa Sweden, aliyewakilisha msismamo wa nchi hizo, alitoa mwito ulioisihi Cuba pia kuhishimu na kutekeleza haki za binadamu, na kupendekeza kwa Serikali ya Cuba kuwaachia kutoka vizuzizini wale wapinzani wasiokubaliana na sera za serikali yao.

Balozi wa Marekani katika UM, Susan Rice, yeye kwa upande wake alilaumu wawakilishi wa Cuba katika Baraza Kuu ambao alisema walitumia lugha yenye maumivu wa ufasaha wa usemaji unaofanana na enzi za vita baridi; na alisisitiza Marekani ina haki ya kimamlaka, kuongoza uhusiano wa kiuchumi kwa kulingana na masilahi ya taifa:

"Uhusiano wa kiuchumi baina ya Marekani na Cuba ni masuala yanayohusu pande mbili hizi pekee, na ni sehemu tu ya orodha ndefu ya masuala yanayoambatana na uhusiano kati ya mataifa. Hatua zilizochukuliwa karibuni na Serikali ya Marekani, kuendeleza mawasiliano na Cuba, na kubadilishana shughuli za kitamaduni baina yao, zimechukuliwa kidhati kwa makusudio ya kuihamasisha Serikali ya Cuba kuhishimu kanuni za kimsingi zilizomo kwenye Mkataba wa Kidemokrasia kwa Mataifa ya Mabara ya Amerika na kwenye Mwito wa Azimio la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu."

Balozi wa Marekani vile vile aliitaka Serikali ya Cuba kuwaachia kutoka kizuizini wafungwa wote wa kisiasa, na kuiomba iidhinishe Mkataba wa Kimataifa juu yaHaki za Kiraia na Kisiasa, na vile vile kuruhusu watetezi huru maalumu juu ya haki za binadamu na mateso, kuzuru magereza ya Cuba.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba alijibu stihizai za madai ya Balozi wa Marekani kwa kuitaka serikali ya Marekani, halkadhalika, iwaachie huru wale raia watano wa Cuba waliotiwa ndani kwenye nagereza ya Marekani, kutumikia vifungo vya muda mrefu, kwa makosa ya kufuatilia makundi ya upinzani ya Wacuba waliopo Marekani, ambayo alisema yamenuia kuendeleza kile alichotafsiri kama ni vitendo vya ugaidi vinavyohatarisha maisha ya umma wa Cuba. Vile vile Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba aliyalaumu mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, yakijumuika na Marekani, kwa vitendo vyao vilivyokiuka sheria ya kimataifa ambapo wanajeshi wao walitesa wafungwa kwenye Vituo vya Jela za Guantanamo na kwenye magereza ya Iraq ya Abu Ghraib.