Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM aomba msaada ziada kuhudumia usalama kwa watumishi wa UM

KM aomba msaada ziada kuhudumia usalama kwa watumishi wa UM

Alkhamisi, KM Ban Ki-moon ametoa onyo lenye kuhadharisha ya kuwa, hivi sasa, watumishi wa UM hivi sasa tumegeuzwa kuwa "walenghwa dhaifu", na yale makundi yalionuia kutuhujumu kihorera, bila kujali adhabu.

Kwa hivyo, KM ameyaomba Mataifa Wanachama kuipatia UM walinzi ziada, kuhami na kuwakinga watumishi wa UM waliopo Afghanistan, pamoja na majengo yao, hasa katika kipindi ambapo taifa hilo, linajitayarisha kufanyisha duru ya pili ya uchaguzi wa uraisi. Alisema UM huenda ikahamisha wafanyakazi wake waliopo kwenye nyumba za wageni, mjini Kabul, na kwengineko nchini, na kuwapeleka kwenye majengo ambayo kutawahakikishia usalama, na kuna uwezekano UM ukalazimika hata kuajiri walinzi kutoka makampuni ya ulinzi, ya binafsi, kulinda watumishi wa UM. KM alibainisha ya kuwa anasubiri kupitishwa ombi la bajeti la kuhudumia shughuli za usalama kwa miaka miwili ijayo, linalokadiriwa dola milioni 471, ikijumlisha ongezeko la dola milioni 40 kwa mwaka huu. Vile vile KM amependekeza kwa Mataifa Wanachama, kupitisha ombi la kuanzisha mfuko wa mipango ya dharura, wa dola milioni 40 zinazohitajika kuhudumia usalama. Baraza la Usalama limeunga mkono ombi la KM la kuongeza usalama na ulinzi kwa wafanyakazi wa UM waliopo Afghanistan. Baraza la Usalama limesisitiza kwenye taarifa yake ya kuwa vurugu na fujo za hapa, pale na kila mahali katika Afghanistan, zisiruhusiwe kabisa kusitisha upigaji kura. Hii leo KM anatazamiwa kuzungumzia Baraza Kuu la UM, ambapo atawakilisha mbele ya wajumbe wa kutoka Mataifa Wanachama 192, mapendekezo kuhusu taratibu zza kuimarisha ulinzi na usalama kwa wafanyakazi wa UM. Wajumbe wa Mataifa Wanachama ndio wenye kudhibiti bajeti la matumizi ya shughuli za UM katika ulimwengu.