Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkariri wa UM anayetetea haki za wateswa amefukuzwa Zimbabwe

Mkariri wa UM anayetetea haki za wateswa amefukuzwa Zimbabwe

Manfred Nowak, Mtaalamu wa UM juu ya masuala ya mateso, na vitendo vyengine visio vya kiutu vyeye kudhalilisha hadhi ya ubinadamu, alkhamisi alitangaza, kutokea Johannesburg, Afrika Kusini ya kuwa ana wasiwasi juu ya madai ya kuwepo hali mbaya, iliokiuka haki za kiutu za wafungwa, katika magereza ya Zimbabwe, taarifa aliowakilisha saa 24 baada ya kunyimwa ruhusa ya kuingia nchini humo kuendeleza uchunguzi kuhusu madai hayo.

Nowak alialikwa rasmi na Serikali ya Zimbabwe, mnamo tarehe mosi Oktoba, kwenda nchini kukusanya ushahidi juu ya madai ya kufanyika vitendo vya mateso, unyanyasaji na hali isio ya kiutu kwenye magereza ya Zimbabwe. Alkhamisi Mtetezi huyu wa Haki za Binadamu wa UM alifukuzwa nchi na kutiwa kwenye ndege iliolekea Afrika Kusini, baada ya kuzuiwa na maofisa wa usalama alipojaribu kuingia Zimbabwe. Alisema kitendo hicho kimesababisha ujumbe wake Zimbabwe kutofanikiwa kutekeleza majukumu yake, kama alivyodhaminiwa na Kamisheni ya Haki za Binadamu. Nowak alinakiliwa akisema kufukuzwa kwake Zimbabwe "kumesitisha ujumbe wake" na alilalamika kwamba aushi wake "hajawahi kutendewa kusiko na adabu, katika kuendeleza shughuli zake, kama alivyofanyiwa na Serikali ya Zimbabwe." Aliahidi kuwa ataliarifu Baraza la Haki za Binadamu juu ya tukio hilo, na atapendekeza kuchukuliwe hatua zinazofaa dhidi ya Zimbabwe.