Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelezo mafupi juu ya mkutano wa kila mwezi wa KM na waandishi habari

Maelezo mafupi juu ya mkutano wa kila mwezi wa KM na waandishi habari

Kadhalika, leo asubuhi, kwenye Makao Makuu ya UM, KM Ban Ki-moon, alifanyisha mazungumzo ya kila mwezi na waandishi habari wa kimataifa.

Alifungua mahojiano kwa kulaani shambulio la nyumba ya wageni waliokuwa wakikaa wafanyakazi wa UM, iliopo mjini Kabul, Afghanistan. Alibainisha watumishi 25 wa UM walisajiliwa kuishi kwenye nyumba ilioshambuliwa na bomu la kujitoa mhanga, ikijumlisha wanaume na wanawake 17 waliowakilisha timu ya kusimamia uchaguzi ya Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP). KM alituma salamu za pole kwa aila zote za watu waliofariki, na pia kwa jamii nzima ya watumishi wa UM. Baada ya hapo KM alizungumzia masuala mengine muhimu yanayotatatnisha walimwengu. Alianza kwa kunasihi juu ya umuhimu wa dharura ya kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni, na alikumbusha kwamba tumebakiza wiki tano tu kabla ya mkusanyiko wa Mkutano Mkuu wa UM juu ya mabadiliko ya hali ya hewa utakaofanyika Copenhagen. Alizihimiza nchi wanachama kuahidi kupunguza haraka tatizo la kumwaga hewa chafu kwenye anga zao. Vile vile alihadharisha kuhusu kupamba kwa matumizi ya mabavu kimataifa, katika kipindi cha karibuni, ambapo alisema mamia kwa mamia ya raia wasio hatia waliuawa na kujeruhiwa kihorera, kwenye mashambulio ya kigaidi, hususan katika Iraq. Alizungumzia vile vile juu ya machafuko yalioshtadi kwenye eneo la Jerusalem Mashariki, liliozunguka Majengo Matakatifu ya Haram Al-Sharif na Hekalu la Mwamba, na alipendekeza vitimbi na mizungu yote ya uchokozi kwenye eneo hilo isitishwe haraka, maana anakhofia bila ya kuyafanya hayo kuna hatari kuu ya vurugu kali kuripuka, ambalo linabashiriwa litaathiri usalama na amani ya jimbo zima la Mashariki ya Kati. Kuhusu ripoti inayojulikana kama Ripoti ya Jaji Goldstone, iliozingatia ukiukaji wa kanuni za kiutu za kimataifa, wakati wa mapigano dhidi ya Tarafa ya Ghaza, yaliotukia mwisho wa 2008 hadi wiki za mwanzo za 2009, KM alikumbusha kwamba waraka huo sasa umepelekewa Baraza Kuu la UM kuzingatiwa na Mataifa Wanachama. Aliongeza kwa kukumbusha pia miezi kumi baada ya uhasama huo kusitishwa Ghaza, vikwazo bado vinaendelea dhidi ya umma wa KiFalastina unaoishi huko; na KM alisema pia zile ahadi za kuchangisha dola bilioni 4.5 zilizotolewa kwenye mkutano wa wafadhili wa kimataifa, uliofanyika Misri siku za nyuma, alisikitika kusema mchango huo umepwelewa na UM haukufanikiwa kushuhudia hata senti nyekundu. Juu ya Iran, KM alisema ukaguzi wa kiwanda kipya cha kusafishia madini ya yuraniamu katika mji wa Qom, unaoendelezwa wiki hii na wataalamu wa Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) ni hatua ya kutia moyo katika kutatua mvutano juu ya mradi wa Iran kuwa na haki ya kuzalisha nishati kwa matumizi ya raia.