Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Mfanyakazi mmoja wa Kituo cha Kufyeka Mabomu Yaliotegwa Cyprus (MACC), raia wa Msumbiji, aliuawa leo kwenye ajali iliotukia wakati akiendeleza operesheni zake. Kifo hiki ni cha kwanza kutukia. katika miaka mitano ya shughuli hizi kisiwani Cyprus. Mwaathirika wa ajali hiyo anaitwa Femisberto Novele, na alifariki baada ya bomu liliotegwa kuripuka, katika milango ya saa mbili za asubuhi, kwenye uwanja ulioambukizwa vijibomu viliotegwa ardhini, karibu na sehemu ya Geri, iliopi kilomita 10 kusini-mashariki ya mji wa Nicosia. Taye-Brook Zerihoun, Mjumbe Maalumu wa UM kwa Cyprus na mkuu wa Vikosi vya UM Kulinda Amani Cyprus (UNFICYP) alisema alishtushwa na kuhuzunishwa na ajali iliosababisha kifo cha Novele, tukio ambalo, alitilia mkazo, lilikuwa ni msiba kwa UM, unaokumbusha hatari wanayokabiliwa nayo wafanyakazi wa kimataifa wanaohudumi ufyekaji wa mabomu yaliotegwa, ambayo yamenea katika sehemu kadha katika Cyprus. Zerihoun aliwatumia mkono wa pole ukoo wa marehemu Novele, kwa niaba ya timu ya watumishi wa UM waliopo Cyprus. Mradi wa MACC husimamiwa na Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) na tangu 2004, wafanyakazi wa Kituo cha MACC walifanikiwa kuondosha na kuangamiza mabomu 14,000 yaliotegwa, na kusafisha maeneo 57 yaliotegwa mabomu, yanayojumuisha kilomita za mraba milioni 6.5 za ardhi.

Asubuhi Baraza la Usalama lilikutana kushauriana kuhusu suala la Sudan na mada nyengine za kimataifa. Ashraf Qazi, Mjumbe Maalumu wa UM kwa Sudan aliwakilisha taarifa inayoelezea maendeleo kwenye shughuli za kuimarisha utulivu na amani nchini Sudan. Vile vile Baraza lilizingatia masuala yanayohusu taratibu za kusawazisha amani Afrika Magharibi na kusailia vurugu lilioibuka karibuni katika Guinea.

Robert Serry, Mratibu Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani kwa Mashariki ya Kati aliwakilisha ujumbe wa UM, kwa niaba ya KM, kwenye Mkutano wa Kimataifa juu ya Jerusalem, unaofanyika mjini Rabat, Morocco. Kwenye salamu alizotuma KM kwenye kikao hicho, alihadharisha ya kuwa mtafaruku uliofukuta na kujiri hivi sasa kwenye mji wa Jerusalem, unahitajia kudhibitiwa mapema, au si hivyo, kuna hatari ya kudhoofisha hali ya kuaminiana inayohitajika kwenye eneo, na athari zake zitadhuru utulivu na amani ya maeneo mbali na hapo. Kwa sababu hii ndio KM alitoa mwito wa kuugeuza mji wa Jerusalem kuwakilisha alama hakika ya amani, na kujumuisha jamii zote za kimataifa ili kuanzisha enzi mpya itakayojenga hali ya masikilizano kwa jimbo zima la Mashariki ya Kati.