Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Baraza la Usalama limekutana leo, awali, kwa mashauriano juu ya Lebanon, na kufuatiwa na mapitio kuhusu vikwazo vilioekewa Cote d\'Ivoire na UM. Ripoti ya mwisho ya Tume Maalumu ya Wataalamu juu ya Cote d\'Ivoire ilithibitisha mzozo wa taifa hili la Afrika Magharibi umeonekana kuchukua sura tofauti, na hauhusu tena mikwaruzano baina ya jimbo la kaskazini na kusini pekee, bali pia inajumlisha makabiliano baina ya wahusika kadha wengineo ambao baadhi yao hupinga rai ya Cote d\'Ivoire kuungana, na wengine wangelipendelea kuona taifa lao linaungana. Ripoti ya Tume ilieleza vile vile eneo la kaskazini linashabihiana, sasa hivi, na mazingira ya uchumi unaoendeshwa na majemadari wa vita (warlords) badala ya sehemu ya taifa ilio chini ya himaya ya serikali. Makamanda wa vita wa kundi la waliokuwa waasi wa Forces Nouvelles wanaosimamia ‘maeneo huru\' wanaoyadhibiti na kunyonya mali ya asili ya Cote d\'Ivoire, ndio sehemu za nchi zinazowachumia mapato. Tume ya Wataalamu ilisema inashughulishwa na tatizo la uhamishaji wa silaha na baruti, pamoja na risasi, kutoka Burkina Faso wanazopelekewa waasi wa Forces Nouvelles, kadhia ambayo Tume ilibashiria hufungamana na biashara ya magendo ya kuuza kakao. Vile vile biashara haramu ya kuuza almasi ilikutikana kufanyika kati ya Cote d\'Ivoire na Burkina Faso na Mali, kwa kupitia Guinea na Liberia, kwa sababu ya ukosefu wa udhibiti wa mipaka baina ya mataifa haya.

Baraza la Usalama linatarajiwa kuzingatia ripoti mpya ya KM kuhusu maendeleo katika utekelezaji wa Mapatano ya Jumla ya Amani (CPA) Sudan Kusini, na operesheni za Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani kwa Sudan Kusini (UNMIS). Ripoti ilieleza ya kuwa maendeleo wastani yalipatikana katika kutekeleza mapatano ya CPA, lakini malengo fulani muhimu yalishindwa kukamilishwa, hususan yale yanayohusu kuitisha uchaguzi na kura ya maoni. UM ulieleza tatizo la kuzuka mapigano ya kikabila yaliotukia mara kwa mara Sudan Kusini katika mwaka huu, na suala la kuenea kwa wingi kwa silaha kieneo, ni mambo yenye kuongeza wasiwasi kuhusu hali ya utulivu na amani ya jimbo hili la Sudan. Kwa hivyo, Serikali ya Khartoum imenasihiwa kuimarisha juhudi za kukomesha vurugu lionalozuka mara kwa mara katika sehemeu hiyo ya nchi, na ilitakiwa iwashike na kuwafikisha mahakamani wale watu wanaohusika na uchokozi wa mizozo hiyo. Ripoti ya KM ilibashiria, mnamo miezi 18 ijayo, raia wa Sudan watakabili masuala magumu, na namna masuala haya yatakavyoshughulikiwa yataamua kama maendeleo ya taifa yatapatikana nchini katika siku za baadaye au la.

Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) limeripoti Ijumatatu watu 10 waliuawa kutokana na mapigano ya kikabila, yaliofumka kwa mara nyengine tena katika eneo la Shangil Tobaiya - liliopo kilomita 70 kusini ya mji wa El Geneina, Darfur Kaskazini. Makabila yaliohasimiana yalijumuisha jamii za Zaghawas na Birgids, ambayo mapigano yao vile vile yalisababisha majeruhi 11. Baadhi ya majeruhi walipelekwa Shangil Tobaiya kwa matibabu na wengine walihamishwa na helikopta na kupelekwa mji wa El Fasher kutibiwa. UNAMID itatuma timu maalumu ya uchunguzi kutathminia hali halisi ya chanzo cha uhasama uliozuka katika Shangil Tobaiya.

Watawala wa Israel wameripotiwa na Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) kushiriki kwenye shughuli za kubomoa nyumba za koo sita za KiFalastina kwenye eneo liliolikaliwa kimabavu la WaFalastina la Jerusalem Mashariki. OCHA imesihi vitendo hivyo ni lazima visitishwe haraka, na bila ya shuruti. Israel imekumbushwa juu ya jukumu lao la kuwapatia raia wa Eneo Liliokaliwa la WaFalastina (OPT) hifadhi wanayostahiki chini ya sheria za kimataifa na kukomesha, halan, uhamisho wa nguvu na unyanganyi wa rasilmali zao. OCHA ilieleleza tukio la Ijumanne limehusisha WaFalastina 26, wakijumlisha watoto wadogo 10. Vitendo hivyo, OCHA ilionya, vya Israel kung'oa kwa nguvu makazi na kubomoa mastakimu ya WaFalastina katika Jerusalem Mashariki na sehemu nyengine za maeneo yaliokaliwa ni mambo yenye kutengua na kubatilisha kihakika sheria ya kimataifa na athari zake, kwa siku za baadaye, zitadhuru zaidi, kihali na kiakili, aila kakdha za KiFalastina na jamii zao, kwa ujumla, katika muda mrefu ujao.