Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ayapongeza Mataifa ya Afrika kwa kuidhinisha chombo kipya cha sheria kulinda haki za wahamiaji wa ndani

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ayapongeza Mataifa ya Afrika kwa kuidhinisha chombo kipya cha sheria kulinda haki za wahamiaji wa ndani

Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu amekaribisha, kwa furaha kuu, maafikiano ya kuwa na mkataba wa kihistoria kuhusu hifadhi ya wahamiaji wa ndani ya nchi katika Afrika, ambao uliidhinishwa leo hii kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa Wakuu wa Mataifa Wanachama wa Umoja wa Afrika unaofanyika Uganda.

Pillay alisema uidhinishaji wa Mkataba wa Kuhifadhi na Kuhudumia Wahamiaji wa Ndani ya Nchi Waliong'olewa Makazi katika Afrika, ni hatua muhimu ya maendeleo ya mbele kabisa katika kukidhia mahitaji ya umma unaonyimwa makazi ndani ya mataifa yao kwa sababu ya maafa, vurugu na misiba ya kimaumbile. Alipongeza na kuingiwa moyo kuona nchi za Afrika zipo msitari wa mbele katika kuanzisha chombo cha sheria ya lazima ili kulinda na kutunza haki za wahamiaji wa ndani ya nchi wa katika bara zima la Afrika. Kama inavyofahamika mamilioni ya raia wa Afrika - katika mataifa ya Chad, JKK, Kenya, Usomali na Sudan - wamenyimwa makazi yao ya kawaida, kwa sababu ya mapigano na magonjwa ya kimaumbile. Umuhimu wa maafikiano haya mapya, yalioidhinishwa na nchi za Afrika, ni kwamba nusu ya watu milioni 26 waliong'olewa makazi duniani hukutikana Afrika.