Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ijumaa usiku KM Ban Ki-moon alifungua rasmi Tafrija ya Muziki kwenye ukumbi wa Baraza Kuu, kuadhimisha Siku Kuu ya UM, ambayo kikawaida, huadhimishwa kila mwaka mnamo tarehe 24 Oktoba. Mwaka huu Siku Kuu ya UM inaadhimishwa Makao Makuu tarehe ya leo kwa sababu, tarehe 24 Oktoba 2009 imeangukia Ijumamosi, ambapo maofisi huwa yanafungwa kwa sababu ya mwisho wa wiki. Mada ya taadhima za mwaka huu ina kaulimbiu isemayo "Tuwahishimu Walinzi Amani". Kwenye risala yake KM alipongeza mchango muhimu wa walinzi amani wa kimataifa, waume na wake 115,000 waliojitolea mhanga kurudisha utulivu na amani katika yale maeneo ya ulimwengu yalioambukizwa na machafuko na hali ya wasiwasi. Alikumbusha walinzi amani wa UM ni miongoni mwa "mabalozi bora kabisa" wa taasisi yetu ya kimataifa.

 Naibu KM juu ya Masuala ya Kisiasa, B. Lynn Pascoe yupo Kenya siku ya leo, akikamilisha ziara maalumu ya mataifa matano yaliopo sehemu za kusini na mashariki katika Afrika. Ziara yake ililenga kutathminia juhudi za kuimarisha ushirikiano bora kati ya UM na mataifa ya eneo, ikijumlisha zile sehemu zilizopambwa na mizozo, hususan Usomali. Leo, mjini Nairobi, Pascoe vile vile alijumuika na Waziri Mkuu wa Usomali kuongoza Kamati ya Cheo cha Juu inayofuatilia utekelezaji wa mapatano ya amani ya Djibouti. Pascoe alitoa mwito maalumu wenye kuhimiza jamii ya kimataifa kuongeza mchango wao wa dharura wa kuisaidia Usomali "kwa vitendo, badala ya kauli pekee", ili iweze kukomesha hali mbaya iliolidhuru taifa hili katika miaka 18 iliopita. Kadhalika, Pascoe alifanya mazungumzo na Raisi Mwai Kibaki wa Kenya katika siku ya leo, na alisema kwenye mazungumzo yao alisisitiza juu ya umuhimu wa kusawazisha amani na kurudisha utulivu Kenya, hali ambayo itasaidia vile vile usalama wa ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Kabla ya hapo Pascoe alizuru Uganda na Burundi, na alipokuwepo huko alizishukuru serikali za mataifa haya mawili kwa mchango wao wa kutuma vikosi Usomali, kujiunga na walinzi amani wa Umoja wa Afrika wa AMISOM. Vile vile kabla ya hapo Pascoe alizuru Afrika Kusini na Angola.

Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA), limeripoti kwamba Iran imeomba ipewe muda zaidi kuzingatia itifaki ya awali iliopendekezwa na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Mohamed El Baradei kuhusu taratibu za kuisaidia Iran kupata nishati itakayotumiwa kwenye kiwanda cha kiraia cha kufanyia utafiti wa matibabu. Ufaransa, Urusi na Marekani nchi ambazo zilishiriki kwenye mazungumzo juu ya suala hilo na IAEA, zimetangaza kuidhinisha mapendekezo ya El Baradei. Lakini Iran imemwarifu Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kwamba "inazingatia, kwa kina, pendekezo lake ambalo wanalipa mwangaza wa upendeleo, na inahitajia kupewa muda zaidi mpaka kati ya wiki ijayo, kabla haijatoa uamuzi wake rasmi."