Walinzi amani wa UNAMID wasaidia kukomesha mapambano ya kikabila Darfur Kaskazini

22 Oktoba 2009

Ofisi ya Msemaji wa KM imeripoti walinzi amani wa Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) walilazimika wiki hii kuingilia kati kuzuia mapambano makali ya kikabila yaliotukia karibu na eneo la Shangil Tobaya, Darfur Kaskazini baina ya makabila ya Zaghawa na Birgid.

Watu wawili waliripotiwa kuuawa na watu sita kutoka makabila yote mawili walijeruhiwa kwenye mapigano, wanne kati ya majeruhi hawo hali yao inasemekana kuwa ni maututi kwa hivi sasa. UNAMID imetumia helikopta zake kuwahamisha majeruhi kupata matibabu kwenye hospitali ya serikali katika mji wa El Fasher, na wengine wamepelekwa kwenye hospitali ya UNAMID. Chanzo cha mapigano haya ya kikabila kinadhaniwa kinatokana na ushindani juu ya nani mwenye haki ya kumiliki vituo vya maji. UNAMID imejaribu kuutatua mvutano huo kwa suluhu ya muda ambapo jamii za makabila husika zitapatiwa maji safi na vikosi vya ulinzi amani vya UM na UA vya UNAMID.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter