Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imetangaza tena ilani ya kuwahadharisha walimwengu kwamba zaidi ya watu milioni 23 wanaoishi katika Pembe ya Afrika, huenda wakaathiriwa na mvua kali na mafuriko yanayoashiriwa kuchochewa na mfumo wa hali ya hewa ya El Nino. Taarifa ya OCHA ilitilia mkazo ya kuwa umma unaokabiliwa na hatari ya kudhurika zaidi na hali hiyo - katika mataifa ya Usomali, Kenya, Uganda, Tanzania na Djibouti na Eritrea na Ethiopia - ni zile jamii zinazojumlisha wafugaji, wakazi wa vijijini, wakulima pamoja na wahamiaji wa ndani na wale wa kutoka nchi za kigeni.

KM ameliarifu Baraza la Usalama kuwa ana azma ya kumteua Liuteni Jenerali Sikander Afzal wa Pakistan, kuwa Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi Amani vya UM Liberia (UNMIL), na atamrithi Liuteni Jenerali A.T.M. Zahirul Alam of Bangladesh aliyemaliza muda wake jana Ijumatatu (19 Oktoba 2009). Kamanda Mkuu mpya wa UNMIL alijiunga na jeshi la Pakistna 1972 na, katika miaka ya 1994 na 1995, aliongoza vikosi vya dharura vya operesheni ya pili ya amani ya UM katika Usomali (UNOSOMII).

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limeanzisha mfumo mpya wa kudhibiti bora misitu katika dunia, wenye lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira ya misitu, kwa ujumla. Mfumo huu utazisaidia nchi wanachama, hasa mataifa maskini, kupatiwa taarifa madhubuti, bila ya malipo, zitakazotumiwa na nchi husika kudhibiti vyema misitu yao, taarifa ambazo zilikusanywa kutoka setilaiti, zenye mchanganuo wa data za hali ya juu kabisa kuhusu mazingira halisi ya misitu. Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Jacques Diouf, alinakiliwa akisema kwamba katika siku za nyuma taarifa hizi zilikuwa hazikabidhiwi, moja kwa moja, mataifa yanayoendelea. Aliongeza kwa kueleza ya kuwa mfumo huo mpya hauna gharama, una usahihi mkubwa na uwazi unaoridhisha kuzisaidia nchi zinazotaka kushiriki kwenye huduma ya kupunguza uharibifu wa mazingira ya misitu.