Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali za Africa zajiendeleza kiutawala, lakini rushwa bado inakithiri, inasema ripoti ya UM

Serikali za Africa zajiendeleza kiutawala, lakini rushwa bado inakithiri, inasema ripoti ya UM

Ripoti mpya ya UM, iliotolewa tarehe 16 Oktoba 2009, kusailia shughuli za utawala katika bara la Afrika, ilibainisha ya kuwa katika miaka minne iliopita, maendeleo machache yalipatikana kwenye viini vya harakati za utawala, na ilidhihirisha, tatizo la ulajirushwa katika Afrika, lilifurutu ada na kuongezeka kwa kiwango kikubwa katika kipindi hicho.

Toleo hili la pili la Ripoti juu ya Utawala katika Afrika, ilioandaliwa na Baraza la UM juu ya Maendeleo ya Uchumi kwa Afrika (ECA), ilikusanyisha maelezo ya jumla kuhusu hali ya utawala katika nchi 35 za Afrika. Ilieleza kiashirio cha udhibiti wa rushwa katika mataifa hayo, kiliteremka kwa asilimia 3 katika miaka minne iliopita, na ilitilia mkazo pia "rushwa ni moja ya vizingiti vikubwa kabisa vyenye kukwamisha juhudi za kuufyeka umaskini na hali duni, na ni tatizo ambalo huwafanya matajiri na wenye kumiliki mitaji kutokuwa na imani ya kuwekeza mali zao kwenye uchumi wa nchi za Afrika na katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani humo." Kadhalika, ripoti ilibainisha licha ya kuwa uchaguzi hufanyika mara kwa mara katika mataifa kadha ya Afrika yaliofanyiwa utafiti, hata hivyo mara nyingi shughuli hizo za uchaguzi hukutikana na dosari na kasoro mbalimbali katika nchi nyingi husika, hali ambayo husababisha hadhi ya uchaguzi kutiliwa mashaka na umma pamoja na waangalizi wa kizalendo na wale wa kutoka nje. Ripoti ilithibitisha vyama tawala huonyesha uhasama, na uadui mkubwa dhidi ya vyama vya upinzani ambavyo hunyimwa fursa halali na uwezo wa kushindana, kwa uwiano unaofaa na bila ya matatizo.