Hapa na pale

Hapa na pale

John Holmes, Naibu KM Mdogo juu ya Masuala ya Kiutu anatazamiwa kufanya ziara maalumu Uganda kuanzia tarehe 20 mpaka 24 Oktoba, ili kuhudhuria Mkutano Mkuu Maalumu wa Umoja wa Afrika (UA) juu ya Wahamiaji, Warudiwaye Makwao na Wahamiaji wa Ndani wa Afrika. Kadhalika, wakati Holmes atakapokuwepo Uganda anatazamiwa kufanya tathmini juu ya hali nchini Uganda, ambapo jumuiya ya wahudumia misaada ya kiutu inashirikiana na Serikali kuhakikisha watu milioni mbili waliong’olewa makazi na mashambulio ya waasi wa kundi la LRA huwa wanapatiwa suluhu na utulivu wa kudumu wa kuridhisha kimaisha.

KM ameshtumu kwa lugha nzito shambulio la magaidi liliotukia Ijumapili katika jimbo la Sistan-Baluchistan, Iran, ambapo imeripotiwa idadi kubwa ya watu walifariki na watu kadha wengine walijeruhiwa. Kwa mujibu wa taarifa ilizopokea UM mshambuliaji mmoja alijiripua wakati baadhi ya wanajeshi Walinzi wa Kimapinduzi walipokusanyika kukutana na jamii na wazee wa makabila ya eneo la kusini-mashariki la Iran. KM aliwatumia mkono wa taazia aila zote za waathirika wa tukio hilo, pamoja na Serikali ya Jamhuri ya KiIslam ya Iran, na aliwaombea majeruhi wapone haraka.

KM amekaribisha ripoti ya kuachiwa huru, Ijumapili iliopita, kwa watumishi wawili wa shirika la kimataifa lisio la kiserikali la GOAL. Watumishi hawa walitoroshwa kimabavu kutoka Darfur, Sudan mnamo tarehe 02 Julai 2009. Kadhalika, KM alipongeza maelfu ya wafanyakazi wa mashirika yanayohudumia misaada ya kiutu Sudan, kwa mchango wao muhimu wa kunusuru maisha ya umma muhitaji. Alikumbusha, dhamana ya ulinzi na usalama wa wahudumia misaada ya kiutu na walinzi amani wa kimataifa imo mikononi mwa Serikali ya Sudan.

Ripoti ya KM juu ya operesheni za Shirika la Ulinzi Amani la UM katika Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINURCAT), iliotolewa karibuni, imeeleza maendeleo ya taratibu yalipatikana kwenye utekelezaji wa madaraka iliodhaminiwa nayo na Baraza la Usalama, ya kueneza kikamilifu hali ya usalama kwenye maeneo ya operesheni zake. Alisema ni muhimu kuishirikisha, kwa usarifu zaidi, Serikali ya Chad na washiriki wenzi, hususan katika kuhudumia wahamiaji wanaorejea makwao kutoka nje na wale wahamiaji wa katika ndani ya nchi. Alieleza hali ya wasiwasi baina ya Chad na Sudan bado inaendelea kusumbua mataifa haya jirani, na alisema jamii ya kimataifa na watendaji wa kikanda ndio wenye uwezo halisi wa kufufua tena juhudi za amani zenye maana kwenye eneo hilo. Alitilia mkazo kwamba amani na utulivu wa muda mrefu wa eneo utategemea, awali, suluhu kwenye mizozo ya ndani ilioselelea ndani ya Chad na Sudan. Ripoti ya KM vile vile alibainisha matatizo mengine yaliotukia kwenye eneo, ikijumlisha tatizo la kuongezeka kwa upatikanaji wa urahisi wa silaha kwenye sehemu za Chad mashariki, na kupamba kwa mizozo ya kikabila, ikichanganyika na hali ya wasiwasi katika sehemu za mipakani, migogoro ambayo ripoti ilionya inachokora zaidi utulivu wa amani na usalama wa jamii.

Kwa mujibu wa taarifa za mwanzo mwanzo zilizopatiwa Vikosi vya Muda vya UM vya Kulinda Amani Lebanon (UNIFIL), ilioripotiwa kwamba katika mwisho wa wiki iliopita miripuko miwili ilitukia Lebanon kusini, na kwa bahati nzuri tukio hili halijajeruhi mtu. Uchunguzi wa awali umeonyesha miripuko ilisababishwa na chaji ya viripuko vya chombo kinachogundua mwanga, kilichotegwa ardhini kwenye eneo hilo na jeshi la Israel wakati wa vita ya 2006. Uongozi wa UNIFIL umeshawasiliana na makundi yote mawili yanayohusika na mgogoro wa 2006. UNIFIL imeanzisha uchunguzi wa kutafuta chanzo halisi cha kuwepo kwa silaha hizi kwenye eneo, ili kuhakikisha namna viripuko hivyo vilivyofyatuliwa na kujua ni nani aliyehusika kihakika na jukumu hilo. Wachunguzi wa UNIFIL sasa hivi wanashirikiana na Vikosi vya Jeshi la Lebanon kukamilisha uchunguzi wao.

UM imeripoti Haile Menkerios, KM Msaidizi juu ya Masuala ya Kisiasa, akiongoza ujumbe maalumu wa UM, kuanzia Ijumaa iliopita alifanya ziara ya kutembelea Guinea na maeneo jirani, Afrika Magharibi ili kutayarisha Bodi la Uchunguzi litakaloendeleza upelelezi kuhusu fujo na vurugu liliofumka nchini Guinea mnamo tarehe 28 Septemba 2009. Leo Ijumatatu, ujumbe uliondoka Conakry kuelekea Ouagadougou, mji mkuuwa Burkina Faso ambapo Menkerios atakutana, kwa mashauriano na Rais Blaise Compaoré, mpatanishi kuhusu Guinea wa Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi kwa Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS).

Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD) limechapisha ripoti mpya yenye kueleza kwamba baadhi ya sekta ya teknolojiya ya mawasiliano ya kisasa (ICT) zimefanikiwa kukabili vyema dhoruba za miporomoko ya shughuli za kiuchumi zilizofumka miezi ya karibuni kwenye soko la dunia, wakati sehemu nyengine za ICT ziliathirika na matatizo ya uchumi na fedha. Ripoti ilisema shughuli za biashara ndogo ndogo katika nchi zenye mapato ya chini, zilionekana kutumia, kwa kiwango kikubwa, simu za mkononi kushinda kompyuta, na kuzimudu simu hizo za mkononi kama ni chombo muhimu cha mawasiliano ya kisasa kinachotumiwa na umma. Matumizi ya simu za mkononi yalikithiri zaidi katika bara la Afrika na kwenye sehemu nyengine za mataifa yanayoendelea. Hata hivyo, ripoti ilisema bado kuna pengo kubwa baina ya nchi tajiri na mataifa maskini katika matumizi ya "intaneti na televesheni za setilaiti", hali ambayo inahatarisha na kutilisha wasiwasi mkubwa kuhusu maendeleo katika mataifa yanayoendelea. Ripoti ya UNCTAD vile vile ilifahamisha kwamba shughuli za Intaneti ni huduma muhimu zenye kumsaidia mfanya biashara wa karne ya sasa kujipatia nguvu na uwezo halisi wa kushiriki kwenye mashindano yanayofaa kwenye soko la kitaifa na kimataifa.