Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tarehe 17 Oktoba inaadhimishwa na UM kuwa ni Siku ya Kimataifa Kuufyeka Umaskini

Tarehe 17 Oktoba inaadhimishwa na UM kuwa ni Siku ya Kimataifa Kuufyeka Umaskini

Mnamo Ijumamosi, tarehe 17 Oktoba, UM utaadhimisha Siku ya Kimataifa Kufyeka Umaskini.

Mtaalamu Huru Maalumu juu ya haki za binadamu na umaskini uliovuka mipaka, Magdalena Sepúlveda, alisisitiza kwamba tunawajibika, kama umma wa kimataifa, hususan katika kipindi kigumu cha hivi sasa, kukumbushana juu ya ulazima na umuhimu wa kufyeka ufukara na hali duni, kote ulimwenguni. Mwaka 2009 tuliarifiwa ni mwaka ambao UM unasema ulimwengu ulishuhudia upotezaji mkubwa wa ajira na kazi, na utapiamlo katika kipindi hiki umefikia kilele kisichowahi kushuhudiwa kihistoria, ambapo watu bilioni moja husumbuliwa na ukosefu wa lishe inayofaa kuishi kibinadamu. Kadhalika, Sepúlveda alisema kwa sababu ya matatizo ya kifedha katika nchi nyingi wanachama, uwekezaji kwenye sekta za ilimu na utunzaji wa afya ya jamii umepungua kwa kiwango kikubwa kabisa, hali ambayo inahatarisha zaidi maisha ya umma maskini, kundi ambalo maisha yao hukorogwa zaidi na janga la mifumko ya bei ya vyakula liliochochewa na migogoro ya kiuchumi ilitifuka katika 2008.