Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti nchi ziliopo kwenye Pembe ya Afrika, ambazo karibuni zilisumbuliwa na ukame wa kihistioria, hivi sasa zinajiandaa kukabilina tena na maafa mengine yanayoletwa na majira ya hali ya hewa ya El Nino, hali ambayo inatarajiwa kuzusha mafuriko makuu kwenye eneo hilo. OCHA ilitahadharisha kuna uwezekano mkubwa mataifa ya Kenya, Usomali, Tanzania na Uganda huenda yakadhurika na miporomoko ya ardhi kwa sababu ya El Nino, mfumo wa hali ya hewa unaotarajiwa pia kuathiri na kuharibu mavuno, kuzusha maradhi yanayosababishwa na maji machafu na kuharibu mitandao ya mabarabara. Kadhalika, OCHA imesema maafa hayo huenda yakadhuru vile vile mataifa ya Djibouti, Eritrea na Ethiopia. John Holmes, Mratibu wa Misaada ya Kufarajia Dharura alidhihirisha ya kuwa watu milioni 23 sasa hivi wanapepesuka, na kusumbuka, na athari za upungufu wa chakula na maji safi na salama, na vile vile wanakabiliwa na uhaba wa maeneo ya malisho ya wanyama, migogoro sugu na hali ya wasiwasi ambayo huathiri sana jamii za wakulima, wafugaji na wale wenye kuishi kwenye mitaa ya mabanda ya vitongoji vya miji mikuu, na huathiri pia wahamiaji wa ndani ya nchi na kutoka mataifa jirani."

 KM Ban Ki-moon ametangaza kuwa ataunda tume maalumu, ya uchunguzi, kutathminia athari za hatua kali za mabavu, zilizochukuliwa mwezi uliopita Guinea na vikosi vya usalama, dhidi ya waandamanji raia, wasiochukua silaha, ambao inakadiriwa 150 ya raia hawa waliuawa, na vile vile wanawake kadha walinajisiwa kihorera na wanajeshi. Lengo hasa la kuunda tume, KM alisema, ni kuchunguza hatua kali za kinidhamu zilizochukuliwa tarehe 28 Septemba katika mji mkuu wa Conakry, na kujaribu kufichua wale wakosa walioendeleza vitendo karaha dhidi ya raia.

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa JKK, na pia mkuu wa Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani (MONUC) asubihi alizungumza mbele ya Baraza la Usalama juu ya maendeleo ya eneo analolishughulikia. Alibashiria utulivu utarejeshwa karibuni ndani ya taifa la JKK. Alisema mgogoro uliolidhuru eneo la mashariki, kwa fafanuzi zake binafsi, unaelekea kukaribia kutia kikomo. Miongoni mwa mafanikio yalioshuhudiwa na MONUC kujiri katika JKK alisema ni matokeo ya kutia moyo ya operesheni za majeshi ya taifa ya FARDC katika majimbo ya Kivu Kusini, Kivu Kaskazini na Orientale, juhudi ambazo zilikomesha kabisa uwezo wa kuanzisha tena fujo kutoka waasi Wahutu wa FDLR na waasi wa Uganda wa LRA.

Adrej Mahecic, msemaji wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) ameripoti wakazi wa jimbo la Waziristan Kusini, katika Pakistan, wiki hii wameanza kuyahama mastakimu, kwa mkumbo unaoshtusha kabisa, kwa matazamio ya kuwa operesheni za kijeshi dhidi ya makundi yanayopinga serikali zinaelekea zitaanzishwa tena na wenye mamlaka. Alisema tangu mwanzo wa Septemba, wahamiaji 80,000 waliong'olewa makazi kutoka Waziristan Kusini walisajiliwa na watawala wa kienyeji wa wilaya za Dera Ismail Khan na Tank kuwasili katika Jimbo la Mpakani la Kaskazini-Magharibi (NWFP). Mnamo mwanzo wa mwaka huu, Wapakistani milioni 2 ziada waling'olewa makazi, baada ya kufumka mapigano baina ya vikosi vya serikali na wapambanaji katika eneo la NWFP, na wingi wa wahamiaji hawa sasa hivi walisharudi makwao. Kwa mujibu wa UNHCR watawala wa serikali za kienyeji wameanza tena kusajili wahamiaji wapya wanaowasili kwenye jimbo la NWFP katika siku za karibuni, na katika siku tatu zilizopita, pekee, familia 800 kati ya 2,000 zilizohamia kwenye eneo hilo zilisajiliwa.

Ofisi ya UM juu ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC) imetangaza ripoti mpya kuhusu biashara ya magendo ya kutorosha watu katika mataifa ya Ulaya. Ripoti iliopewa jina la "Uchambuzi wa Biashara ya Kutorosha Wanadamu Ulaya" ilionyesha watu wachache wanaoshiriki kwenye biashara haramu ya kutorosha wanadamu hushikwa na kushtakiwa katika mahakama za nchi za Ulaya, tukilinganisha na idadi kubwa ya wahalifu wanaokamatwa kwa makosa ya kuteka nyara wanadamu, jinai ambayo hutukia kwa nadra katika maeneo hayo. Ripoti ilisema katika kila watu 100,000 wanaofungamana na biashara ya kutorosha wanadamu ni mtu mmoja tu kati ya jumla hiyo anayefanikiwa kutiwa hatiani katika mataifa ya Ulaya. Ofisi ya UNODC imesema hatua ya kwanza muhimu inayohitajika kuchukuliwa na maatifa husika kukabili makosa haya yanayovuka mipaka ni kwa mataifa kuanza kubadilishana taarifa za kufuatilia, na kuwadhibiti kipamoja wakosa wanaoendeleza magendo ya kutorosha wanadamu wanaonyakuliwa makwao, na kupelekwa nchi za kigeni kushiriki kwenye vibarua vya lazima haramu, hasa vitendo vya umalaya.

KM Ban Ki-moon leo amezuru Skuli ya Kimataifa ya UM (UNIS) iliopo jijini New York, na alipokuwepo huko alichukua fursa ya kuwahamasisha wanafunzi kujihusisha na miradi ya kupambana na ufukara uliovuka mipaka, janga ambalo huathiri watu bilioni moja ziada katika sehemu mbalimbali za dunia. Alisema moja ya njia ya kudhibiti vyema janga la umaskini ni kuhakikisha mitaji maridhawa inaekezwa kwenye maendeleo ya watoto, na Mataifa Wanachama pia yalitakiwa yahakikishe haki za watoto huwa zinahishimiwa na kutekelezwa kama inavyopasa. Ziara ya KM kwenye skuli ya UNIS ilifungamana na ule mradi wa UM wa kupunguza umaskini, wenye mwito usemao "INUKA KUPAMBANA NA UMASKINI".