Mahakama ya ICC inazingatia matukio ya karibuni Guinea

Mahakama ya ICC inazingatia matukio ya karibuni Guinea

Luis Moreno-Ocampo, Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa juu ya Makosa ya Jinai ya Halaiki (ICC) leo amenakiliwa akithibitisha ya kuwa Ofisi yake imeanzisha uchunguzi maalumu kuhusu tukio la Guinea, ambapo mwezi iliopita waandamanaji wa upinzani, wanaokadiriwa 150 waliuawa huko na vikosi vya usalama, pale walipokusanyika kwenye mkutano wa hadhara.

Uchunguzi wa awali wa Mahakama ya ICC unajaribu kuthibitisha ikiwa tukio hili linahitajia kufunguliwa kesi. Kwa mujibu wa Ocampo taifa la Guinea ni miongoni mwa Mataifa ambayo, kuanzia tarehe 14 Julai 2003, yaliridhia na kuidhinisha Mkataba wa Roma, unaoipa Mahakama madaraka ya kusikiliza kesi za kuamua kama kumefanyika makosa ya vita, jinai dhidi ya utu na mauaji ya halaiki yalioendelezwa na raia, ikijumlisha mauaji ya raia na vitendo karaha vya kunajisi kimabavu wanawake kwenye Mataifa yaliotia sahihi Mkataba, ikijumlisha Guinea.