Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Tarehe ya leo, kwa mwaka wa pili mfululizo, inaadhimishwa kimataifa kuwa ni ‘Siku ya Kukumbushana Kuosha Mikono Duniani\', siku ambayo inahishimiwa na Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwea Watoto (UNICEF). Kwenye taarifa iliotolewa na UNICEF ilitilia mkazo umuhimu wa watu kuosha mikono kwa maji safi na sabuni, na kukumbusha kadhia hii ni mojawapo ya huduma za afya kinga zenye matokeo yanayoridhisha, hali ambayo kila mwanadamu anaimudu bila ya gharama kuu.

Wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu Alkhamisi walikutana Geneva, kwenye kikao maalumu, kuzingatia "utekelezaji wa haki za binadamu katika Maeneo Yaliokaliwa ya WaFalastina na juu ya hadhi ya Jerusalem ya Mashariki." Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu alisihi kwenye risala aliowasilisha mbele ya kikao hicho maalumu kusitishwa, haraka, "mawimbi ya amri za kufukuza na kuwatoa WaFalastina kutoka maskani yao halali ambapo nyumba zao hubomolewa kihorera kwenye eneo la Jerusalem Mashariki." Pillay alisema anatafsiri vitendo hivyo dhidi ya raia WaFalstina vinaharamisha sheria za kiutu za kimataifa. Vile vile alitilia mkazo kuwa anaunga mkono mapendekezo na maamuzi ya tume ya kuchunguza ukweli wa mapambano ya Tarafa ya Ghaza, iliyoongozwa na Jaji Richard Goldstone wa Afrika Kusini. Alisisitiza kwamba ni muhimu kwa makundi husika yote na mzozo wa Ghaza kufanyisha, haraka, uchunguzi ulio huru, usiopendelea, na wenye nguvu ya kisheria kuhusu matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu na uharamishwaji wa sheria ya kiutu, yaliodaiwa kutendeka, kwa kulingana na makubalianao na viwango vya maadili ya kimataifa.

Asubuhi Baraza Kuu la UM limeteua wajumbe wapya watano watakaowakilisha Mataifa Wanachama yasio ya kudumu kwenye Baraza la Usalama kwa 2010 na 2011. Mataifa yenyewe ni Bosnia na Herzegovina, Brazil, Gabon, Lebanon na Nigeria. Kadhalika, baada ya mashauriano, wajumbe wa Baraza la Usalama alasiri walifanyisha kikao cha hadhara kusailia hali Kosovo. Mkuu wa Shirika linalosimamia Ujumbe wa UM Kosovo, Lamberto Zannier alihutubia wajumbe wa Baraza kuhusu maendeleo ya karibuni kwenye eneo hilo.

Naibu KM juu ya Misaada ya Dharura, John Holmes leo amemaliza ziara ya siku mbili kutathminia hali Indonesia baada ya kupiga tetemeko la ardhi huko katika tarehe 30 Septemba 2009. Holmes alipata fursa ya kuonana, kwa mazungumzo na ushauriano, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, wafadhili wa misaada ya dharura waliopo nchini, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Usimamizi wa Maafa ya Kitaifa. Vile vile Holmes alikutana na watumishi wa mashirika ya UM na maofisa wengine wanaowakilisha jumuiya za kizalendo zinazohudumia misaada ya kiutu. Makadirio ya mwanzo juu ya mahitaji ya chakula na lishe katika Mji wa Padang, yamebainisha watu 190,000 wanaoishi katika maeneo yalioathirika zaidi na zilzala, wanakabiliwa sasa hivi na upungufu wa chakula kikuu kama mchele. Shirika la Miradi ya Chakula (WFP) linaendeleza kwa sasa ugawaji wa biskuti za lishe bora kwa watoto wa chini ya umri wa miaka 5, pamoja na mama wajawazito na wanawake wanaonyonyesha.

Tarehe 15 Oktoba inatambuliwa na UM kuwa ni Siku Kuu ya Kimataifa kwa Wanawake wa Vijijini. Kwenye risala alitoa KM juu ya siku hii alipendekeza kwa mataifa yote kuhishimu kikamilifu haki za wanawake wa vijijini, pamoja na kuyatekeleza malengo ya miradi ya kuwapatia madaraka wanawake, na aliitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza bidii ya kuyajumuisha mapendekezo haya kwenye ajenda zake juu ya maendeleo. Alisema walimwengu wanawajibika kutambua mchango adhimu wa wanawake wanavijiji katika kuimarisha maendeleo yanayojiendeleza, na katika utunzaji, unaoaminika, wa rasilmali za kizalendo. KM alisema amesikitishwa kuona asilimia kubwa ya wanawake huwa wananyimwa haki halali ya kustarehea ustawi wa kijamii. Ametoa mwito maalumu kwa nchi wanachama kuwekeza zaidi kwenye mitaji ya msingi, na miundombinu itakayowafarajia wanawake wanavijiji kihali, na kuwapunguzia mzigo wa kazi, na wakati huo huo kuwapatia fursa wa kutumia wakati walionao na nguvu walizonazo kwenye soko la ajira na maisha ya umma wa kimataifa.