Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Kimataifa Kupunguza Maafa

Siku ya Kimataifa Kupunguza Maafa

Tarehe 14 Oktoba huadhimishwa na UM, kila mwaka, kuwa ni Siku ya Kimataifa Kupunguza Maafa (ISDR). Kampeni ya mwaka huu ya kuihishimu siku hiyo inalenga shughuli na taadhima zake zaidi kwenye juhudi za "kuzikinga hospitali na madhara ya maafa ya kimaumbile".

Risala ya KM kuhusu Siku ya Kimataifa Kupunguza Maaafa imekumbusha kwamba majanga yanapozuka, hospitali huwa ndio miundombinu muhimu kabisa inayohitajika wakati huo kuokoa maisha ya umma muathirika. Taarifa iliotolewa Geneva na UM kuhusu Siku ya Kupunguza Maafa ilitahadharisha kwamba misiba ya kimaumbile, iliopiga maeneo ya Asia na Pasifiki mnamo mwezi huu, imeonyesha dhahiri kwamba walimwengu tunahitajia kuipatia sekta ya afya hifadhi bora dhidi ya maafa ya kimaumbile, hasa yale majengo ya hospitali na vituo vya matibabu, kwa sababu bila ya kuyafanya hayo kuna hatari ya mateso na usumbufu wa majanga hayo kudhuru halaiki ya umma, ambao kikawaida huwa unategemea huduma za afya za dharura wakati maafa yakizuka. Majengo ya hospitali, zahanati na vituo vyenginevyo vya afya ndivyo vinvyotumiwa kuokoa maisha wakati wa maafa, na ni vyombo vinavyohitajia ulinzi na hifadhi bora ili kuhudumia umma vizuri zaidi wakati wa dharura.