Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO/WFP zahadharisha, mizozo ya uchumi huifanya hali dhaifu ya chakula duniani kuwa mbaya zaidi

FAO/WFP zahadharisha, mizozo ya uchumi huifanya hali dhaifu ya chakula duniani kuwa mbaya zaidi

Ripoti ya pamoja ya mashirika mawili ya UM yanayohusika na miradi ya chakula na kilimo, yaani FAO na WFP, iliotolewa leo Ijumatano, imeeleza kwamba mzozo wa uchumi uliopamba ulimwenguni kwa sasa ndio uliopalilia tatizo la njaa duniani, kwa kiwango cha hali ya juu kabisa cha kihistoria, ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu 1970.

Ripoti hii ya UM yenye mada isemayo Hali ya Chakula Isio Salama kwa 2009, ilibainisha takwimu zenye kuonyesha watu bilioni 1.02  ulimwenguni sasa hivi hukosa chakula cha kutosha, na huwakilisha sudusi moja ya umma mzima wa kimataifa, yaani sawa na mtu mmoja kwa kila watu sita wanaoishi ulimwenguni, idadi ambayo mwaka jana ilikithiri kwa watu milioni 100 ziada. Ripoti ilisema karibu jumla yote ya watu waliokosa chakula cha kutosha duniani hukutikana kwenye yale maeneo ya mataifa yanayoendelea. Takwimu za ripoti zimekadiria watu waliokosa chakula cha kutosha katika maeneo ya Asia na Pasifiki ni sawa na milioni 642. Watu milioni 265 wamekutikana kusumbuliwa na njaa kwenye ukanda wa Afrika, kusini ya Sahara; wakati wakazi milioni 53 huteswa na ukosefu wa chakula cha kutosha katika nchi za Amerika ya Latina/Kusini na maeneo ya Karabiani. Kadhalika, watu milioni 42 wamekadiriwa hukabiliwa na uhaba wa chakula katika eneo la Mashariki ya Karibu na Afrika Kaskazini. Halkadhalika, imethibitishwa watu milioni 15 wanateswa na matatizo ya ukosefu wa chakula kwenye nchi zenye maendeleo ya viwanda, yaani mataifa yaliyoendelea.