Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Naibu KM juu ya Masuala ya Kisiasa, B. Lynn Pascoe anatazamiwa kufanya ziara ya wiki moja katika kusini na mashariki ya Afrika kuanzia tarehe 15 mpaka 23 Oktoba, kwa madhumuni ya kuimarisha uhusiano bora na Mataifa Wanachama pamoja na mashirika ya kikanda, hususan kwenye zile juhudi za kuwahi kuzuia mizozo kabla haijafumka au kuripuka kwenye maeneo hayo, na katika kuimarisha amani na ujenzi wa mazingira ya utulivu baada ya kusitishwa mapigano kwa mafanikio. Miongoni mwa mataifa atakayozuru Pascoe inajumlisha Afrika Kusini, Angola, Burundi, Kenya na Uganda. Vile vile ofisa huyu wa UM atakutana, kwa mashauriano, na viongozi wa maeneo anayoyazuru kuhusu Rwanda, hali katika JKK, maeneo yaliodhurika na mashambulio ya kundi la waasi wa Uganda wa Lord Resistance Army (LRA) na vile atajadilia nawo juu ya utekelezaji wa mpango amani katika Bukini. Zaidi ya hayo Pascoe atakuwa na mikutano, ya vyeo vya juu, na wawakilishi wa kiserikali na wale wanaojumlisha mashirika yasio ya kiserikali; na baadaye atazuru Bujumbura, Burundi yalipo makao makuu ya shirika la UM la ujenzi wa amani la BINUB, na vile vile kuzuru Ofisi ya UM juu ya Masuala ya Kisiasa kwa Usomali (UNPOS) iliopi Nairobi, Kenya.

Baraza la Usalama leo liliitisha kikao cha mara kwa mara, kuzingatia hali ya Mashariki ya Kati. B. Lynn Pascoe, Naibu KM juu ya Masuala ya Kisiasa alipohutubia kikao alibainisha ya kuwa hakuna maendeleo ya kutia moyo yaliopatikana Mashariki ya Kati mwezi uliopita, na badala yake hali ilioshuhudiwa wakati huo kwenye ardhi ya eneo ilikuwa ni ya kutia wasiwasi. Alimaanisha hali inayobashiria mripuko wa mtafaruku hatari unaofukuta sasa hivi katika eneo la Jerusalem Mashariki, liliozunguka Majengo Matakatifu ya Haram al Sharif na Hekalu la Mwamba, kufuatia uvumi wa shughuli zinazoendelezwa na Waisraili kwenye eneo hilo, ambazo zilizusha mapambano baina ya umma wa Falastina na polisi wa Israel. Alisema hadhi ya Mji Mkongwe wa katika Jerusalem, pamoja na majengo ya kidini ni masuala yenye hisia kubwa miongoni mwa wafuasi husika, na suluhu yake inasubiri kuzingatiwa kwenye mazungumzo ya mwisho ya kuchanganua hadhi ya Jerusalem. Kwa hivyo, Waisraili na WaFalastina walinasihiwa kutoanzisha vitendo vya uchokozi utakaochafua mwelekeo huo. Kadhalika, Israel ilinasihiwa kukomesha ujenzi wa makazi mapya ya walowezi kwenye maeneo ya WaFalastina waliokaliwa kimabavu. Juu ya maamuzi ya ripoti ya Tume ya Uchunguzi ya Jaji R. Goldstone kuhusu mashambulio ya Tarafa ya Ghaza, Pascoe alisema KM anaunga mkono hitimisho la ripoti ya Tume, na ameyataka makundi yote husika kuendeleza uchunguzi unaoridhisha, na unaoaminika, bila kuchelewa, kuhusu vitendo vya wafuasi wao wakati wa mapigano. Alieleza hali katika Ghaza, kwa hivi sasa ni isiokubalika kwa sababu ya zingio na vikwazo dhidi ya eneo hili, na ni hali isioweza kuendelezwa wala kusarifika. Aliongeza kwa kubainisha kuvunjika moyo kwa KM kwa ombi lake kukutaliwa na Waziri Mkuu wa Israel, ambapo Ban Ki-moon alipendekeza zana za kujengea maskuli na nyumba zilizobomolewa na mashambulio ya makombora na mabomu pamoja na vifaa vya kujengea zahanati viruhusiwe kuingia Ghaza. Vile vile Pascoe alizungumzia juu ya Lebanon ambapo alihimiza kuundwa kwa serikali mpya ili watakaochukua madaraka watapata fursa ya kushughulikia kidharura masuala yaliozorota nchini yenye kuhusu uchumi, siasa, jamii na usalama.

Shirika la UM juu ya Miradi ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) leo limewasilisha ripoti iliothibitisha kuwa bahari kuu ziliozotunzika na uharibifu wa kimazingira, huwa na uwezo mkubwa wa kupambana vyema na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa. Ripoti inakadiria hewa chafu inayomwagwa kwenye anga - sawa na nusu ya hewa chafu inayomwagwa kila mwaka na sekta ya usafiri - hunasawa kwenye mfumo wa ikolojia ya bahari kuu. Lakini ripoti ilihadharisha vile vile mfumo huo muhimu wa ikolojia ya bahari umeonekana kuanza kuchafuliwa na kuharibika kwa kasi kutokana na athari ya mabadiliko hayo. Bayana hiyo ndio ilioifanya UNEP kupendekeza kwa Serikali wanachama kuwekeza zaidi mitaji yao kwenye huduma za kufufua mifumo maumbile ya bahari kuu na pia kutunza ikolojia yake muhimu kwa masilahi ya umma wote wa kimataifa.