Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makumi elfu ya wahamiaji wa ndani Kivu Kaskazini warudi makwao

Makumi elfu ya wahamiaji wa ndani Kivu Kaskazini warudi makwao

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeeleza kwenye ripoti iliotolewa leo hii ya kwamba tangu maafikiano ya amani kutiwa sahihi, mnamo mwezi Machi 2009, na makundi yanayohusika na uhasama uliopamba katika jimbo la Kivu katika JKK, watu 160,363 walion\'golewa makazi baada ya kuishi kwa muda na aila zilizowapokea, na waliokuwa wakiishi "rasmi" kwenye kambi sita za wahamiaji wa ndani katika mji wa Goma, waliripotiwa kurejea makwao.

Jumla hiyo inawakilisha asilimia 90 ya watu waliokuwepo kwenye kambi hizo za muda za wahamiaji wa ndani ya nchi katika JKK. Wahudumia misaada ya kiutu wameshangazwa na kasi ya uhamisho wa ghafla walioshuhudia kutukia katika siku za karibuni Kivu Kaskazini. Lakini hata hivyo, OCHA imeripoti watu milioni 1.1 walion'golewa makazi, waliopo kwenye jimbo la Kivu, bado wataendelea kuhitajia kufadhiliwa misaada ya kiutu pale watakapoanza kurejea makwao katika miezi michache ijayo. Kwa mujibu wa taarifa ya Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) katika JKK, yaani Pierette VU THI, watu 91,000 bado wamenaswa kwenye zile kambi za wahamiaji wa ndani za dharura, ambapo "watoto dhaifu huathirika zaidi kihali baada ya kutengwa kutoka familia zao, na ambapo watoto wa kike na wanawake watu wazima huhatarishwa zaidi na vitendo karaha vya kunajisiwa kimabavu, na ukandamizaji wa kijinsiya wangali wakisubiri kurejea makwao."