Hapa na pale
Matokeo ya uchunguzi uliondelezwa bia na UM pamoja na Baraza la Mataifa ya Ulaya juu ya biashara haramu ya kuuza viungo, tishu za mwili na chembe za uhai, ambayo hujulikana kwa umaarufu kama biashara ya OTC, yamethibitisha kwamba walimwengu wanahitajia, kidharura, kuunda mkataba mpya, wa lazima, wa kimataifa ili kuzuia biashara ya magendo ya kuuza viungo vya wanadamu, na kuhakikisha waathirika wa jinai hii watalindwa kisheria, na kwa wakati huo huo kuhakikisha wakosa watafikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kuendeleza unyonyaji wa watu maskini na mafukara kwa kuwalazimisha kuuza viungo vyao kufanya pesa. Utafiti umependekeza kupiga marufuku, halan, biashara hii ya kufanya fedha kwa kuuza viungo vya kutoka mwili wa mwanadamu, na ilitaka kuundwe sheria itakayotumiwa kama ndio kigezo cha kusimamia kanuni zinazohusika na uhamishaji wa kiungo cha mwili wa mwanadamu, na wakati huo huo kuhamasisha watu kuamua kujitolea viungo, kwa hiyari, wakifariki, ili kusaidia kuongeza akiba ya viungo hivyo kwenye mahospitali, hali ambayo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa viungo hivyo katika shughuli za matibabu. Mshauri Maalumu wa KM juu ya Masuala ya Kijinsiya na Maendeleo ya Wanawake, Rachel Mayanja aliwaambia wajumbe wa kimataifa waliokusannyika hii leo Makao Makuu kwamba alitumai Baraza Kuu la UM litaandaa haraka msingi wa mkataba wa kupiga marufuku biashara haramu ya viungo kimataifa kwaminajili ya masilahi ya umma maskini.
Ijumanne, watu 500, ikijumlisha wanadiplomasiya, maofisa wa Serikali ya Pakistan na wale wa UM wa vyeo vya juu, pamoja na wafanyakazi wa UM, aila zao na marafiki walikusanyika kwenye ibada maalumu ya kumbukumbu ya kuhishimu wale watumishi wa Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) watano waliouawa kwenye shambulio la bomu la kujitoa mhanga liliofanyika tarehe 05 Oktoba, kwenye Makao Makuu ya Ofisi ya Islamabad ya WFP, ikijumuisha vile vile wafanyakazi wengine wanne waliojeruhiwa, na mmoja wao akiripotiwa hali yake kuwa ni taabani. Risala aliotuma KM kwenye taadhima hizo ilikumbusha ya kuwa waathirika wa shambulio hilo lisio na maana, walikuwa ni wahudumia misaada ya kiutu waliopo msitari wa mbele katika shughuli za kuwapunguzia njaa na maafa umma dhaifu na maskini katika Pakistan, kwa kuendeleza shughuli zao bila ya uchofu. Alisema mchango wa kuwapatia wenye njaa chakula, bila kujali maslahi ya binafsi, ni kadhia ambayo haistahiki hata kidogo kumaanisha kitendo cha kuhatarisha maisha. Aliahidi kwamba hakuna kitakachouzuia UM kutekeleza majukumu yake katika kuhudumia kihali umma muhitaji wa ulimwengu; na alihadharisha kwamba tutaendelea kuwa macho kukabili hatari zote ziliopo katika ulimwengu wa sasa, kwa kutilia mkazo umuhimu wa kuyakamalisha maadili ya UM kama ilivyopendekezwa na Mkataba wa UM.
Bendera ya UM leo ipo nusu mlingoti kwa makusudio ya kuwahishimu askari walinzi amani 11 wa UM, waliouawa Ijumaa iliopita nchini Haiti. Asubuhi, katika mji wa Port-au-Prince, Shirika la UM la Kurudisha Utulivu Haiti (MINUSTAH) lilifanyisha ibada maalumu ya kuwakumbuka walinzi amani hawo, iliohudhuriwa na mamia ya watumishi wa UM, raia wa Haiti na watu wa vyeo vikubwa wa kimataifa. Hédi Annabi, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Haiti alisoma risala alioituma KM iliokumbusha kwamba msiba wa Haiti, uliosababishwa na ajali ya ndege, umethibitisha ya kuwa juhudi za kutunza amani za UM zimejaa hatari zisiotazamiwa, hata kwenye mazingira ambapo mapigano na uhasama huwa yamekosekana. Alisema walinzi amani waliofariki, watano kutoka Jordan na wenziwao sita kutokea Uruguay, walijiaminisha kuelekea maeneo mbali na mataifa yao kuhudumia maadili ya UM yanayotuunganisha sisi sote kama aila moja ya wanadamu.
Asubuhi wajumbe wa Baraza la Usalama wamepitisha, kwa kauli moja, azimio la kuongeza muda wa operesheni za Shirika la UM la Kurudisha Utulivu Haiti (MINUSTAH) kwa mwaka mmoja zaidi, mpaka 15 Oktoba 2010. Kadhalika, wajumbe wa Baraza waliidhinisha pendekezo la KM la kubakiza idadi ya vikosi vya MINUSTAH kwa jumla iliopo hivi sasa, na waliahidi kufanya marekibisho pindi hali katika ardhi itahitajia magheuzi hayo. Kadhalika, Baraza la Usalama limeongeza kwa mwaka mmoja muda zaidi kazi za Tume ya Wataalamu wanaohusika na vikwazo dhidi ya Sudan. Baada ya hapo Baraza la Usalama liliitisha kikao cha faragha ambapo wajumbe wake walisikiliza ripoti ya Choi Yong-jin, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Cote d'Ivoire kuhusu kazi za Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani Cote d'Ivoire (UNOCI).