Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM asema Mpango wa Utendaji wa Cairo juu ya uzazi bora bado haujatekelezwa kama inavyostahiki

KM asema Mpango wa Utendaji wa Cairo juu ya uzazi bora bado haujatekelezwa kama inavyostahiki

Baraza Kuu la UM limeadhimisha leo hii miaka 15 tangu Mkutano wa Kimataifa juu ya Udhibiti wa Idadi ya Watu na Maendeleo uliofanyika Cairo katika 1994 kupitisha Mradi wa Utendaji wa Cairo.

Kwenye risala aliowakilisha asubuhi KM Ban Ki-moon kwenye ukumbi wa Baraza Kuu, aliwaeleza wajumbe wa kimataifa kwa kuwakumbusha ilikuwa ni kikao cha Cairo ambapo serikali za kimataifa zilikiri rasmi, kwa mara ya kwanza, kwamba kila mtu, binafsi, ana haki ya kuwa na afya bora ya uzazi na afya ya kijinsiya. Alisema ni kweli maendeleo kadha yalikwishapatikana ulimwenguni katika kuimarisha afya ya wanawake tangu kikao cha Cairo kilipokamilisha mijadala yake, lakini, hata hivyo, alisema makubaliano yaliofikiwa na wajumbe wa kimataifa katika Misri, hayakufanikiwa kukamilishwa kama inavyotakikana na badala yake yamesalia kuwa ni malengo ya kufikiwa na sio hali halisi ilivyo kuhusu haki ya wanawake. Alisisitiza KM, kwa walimwengu kuweza kukamilisha Mradi wa Utendaji wa Cairo, wanawake wa kimataifa watahitaji kufadhiliwa huduma za afya ya uzazi kwa ukamilifu, ikijumlisha uzazi wa majira, na pia kuwasaidia kwenye zile juhudi za kuufyeka ufukara na hali duni, na kukomesha kabisa vitendo karaha vya kunajisi wanawake na watoto wa kike kwenye mazingira ya mapigano na uhasama, na vile vile kusitisha, halan, tabia ya kuendeleza makosa ya kijinsiya bila ya kukhofu adhabu.