Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Diouf afungua kikao muhimu cha kuzingatia akiba ya chakula duniani katika 2050

Diouf afungua kikao muhimu cha kuzingatia akiba ya chakula duniani katika 2050

Ijumatatu kwenye mji wa Roma, Utaliana, Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limeanza majadiliano ya siku mbili kuzingatia hali ya chakula ulimwenguni katika miaka 40 ijayo.

Kwenye hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Wataalamu wa Hadhi ya Juu Kuhusu Namna ya Kuulisha Umma wa Kimataifa katika 2050, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Jacques Diouf aliwaambia wajumbe wataalamu 300 waliohudhuria kikao, kwamba sekta ya kilimo itahitajia kukuzwa haraka kimataifa ili iweze kuzalisha kwa wingi zaidi chakula kinakachohitajika kulisha umma wa kimataifa katika 2050, umma ambao unabashiriwa utakithiri kutoka idadi ya sasa ya watu bilioni 6.7 na kufika watu bilioni 9.1. Muongezeko huu wa umma utahitajia uzalishaji wa mavuno ya katika kilimo kwa asilimia 70. Diouf alisema mchanganyiko wa ongezeko la idadi ya watu, na kuzidi kwa mapato pamoja na uhamiaji wa kwenye miji kutoka mashamba ni mambo yatakayosababisha mahitaji ya chakula, pamoja na lisha na makapi ya chakula, kukithiri kwa mara mbili. Alihadharisha vile vile upungufu wa mali ya asili kama ardhi, maji safi na viumbehai anuwai, ni mambo yatakayoshinikiza sekta ya kilimo, takriban kote ulimwenguni, kukabili athari zinazoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa; hasa ongezeko la joto, mvua kubwa za kigeugeu na hali ya hewa haribifu isiofuata majira mbayo huzusha mafuriko na ukame usio wa kawaida.