Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM amewasishi wajumbe waliohudhuria Mkutano wa "Mwito wa Cotonou" uliofanyika Ijumatatu, tarehe 12 Oktoba kwenye mji wa Cotonou, Benin, kuzingatia hatari ya biashara ya magendo ya dawa za bandia, kuuhifadhi umma wao na "madhara ya siri na uharamu" wa biashara hiyo. Risala ya KM ilisomwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la UM juu ya Maendeleo ya Uchumi kwa Afrika (ECA), Abdoulie Janneh, na iliyahimiza Mataifa Wanachama "kuunganisha uwezo wao kipamoja kupiga vita jinai ya dunia ya kuuza dawa bandia kwa minajili ya masilahi ya afya ya jamii ya kimataifa." Mradi huu wa kampeni ya kuamsha hisia za kimataifa dhidi ya biashara haramu ya dawa za bandia ni uvumbuzi uliobuniwa na raisi mstaafu wa Ufaransa, Jacques Chirac.

Ijumapili, John Holmes, Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu na Mratibu wa UM Kufarajia Misaada ya Dharura alikamilisha ziara ya siku tatu Yemen. Kabla ya kumaliza ziara yake hiyo, alikutana na Raisi Ali Abdullah Saleh wa Yemen pamoja na viongozi wengine wa vyeo vya juu wa serikali, na aliwaelezea wasiwasi wa UM kuhusu kushindwa kwa wahudumia misaada ya kiutu kuufikia ule umma uliopo maeneo ya mbali ya nchi, hasa wale raia walionaswa kwenye eneo la uhasama. UM umeripoti maelfu ya raia, hususan wale wanaoishi katika Jimbo la Sa'ada, sasa hivi wanakabiliwa na vitisho vya kufanyiwa fujo na vurugu, katika wakati ambao bei za nishati na chakula zinaendelea kuongezeka, na huduma za afya kufifia, hali ambayo inaongeza hatari ya maradhi ya kuambukiza kuripuka kihorera kwenye eneo, hasa ilivyokuwa vituo vyingi vya kuhudumia afya vimesita kufanya kazi kwa sasa. Holmes alisema asilimia 80 ya watu waliong'olewa makazi Yemen kwa sababu ya mapigano, hujumlisha wanawake na watoto wadogo wenye hali dhaifu. Alisihi makundi yote yanayohusika na mgogoro Yemen kuwahakikishia raia kuwa wanapatiwa ulinzi na hifadhi inayofaa, kwa uwiano na kanuni za kimataifa juu ya hifadhi ya raia kwenye hali ya mapigano; na kupendekeza kwa mashirika ya UM kuruhusiwa haraka, na bila vizingiti, kuwafikia waathirika wanaohitajia misaada ya kihali; na pia kuruhusu raia kuhama kutoka maeneo yasiokuwa na usalama bila matatizo.

Ijumanne asubuhi Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani Haiti (MINUSTAH) linatazamiwa kuongoza ibada maalumu mjini Port-au-Prince, ya kuwakumbuka na kuhishimu walinzi amani 11 waliofariki Ijumaa iliopita kwenye ajali ya ndege iliotukia milimani katika kusini-mashariki ya Haiti. Maiti za walinzi amani hawo - sita kutoka Uruguay na watano kutokea Jordan - zitarejeshwa makwao baada ya ibada ya kumbukumbu. Eneo la ajali, liliopo sehemu ya Fonds-Verrettes linalindwa hivi sasa na vikosi vya MINUSTAH, na kunatarajiwa kufanyika uchunguzi juu ya chanzo cha ajali mnamo wiki wiki chache zijazo.

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afghanistan, Kai Eide kwenye mahojiano aliofanya Ijumapili na waandishi habari Kabul, alisema mfumo mgumu wa uchaguzi wa uraisi uliotumiwa majuzi kuendesha upigaji kura nchini Afghanistan, uliharibiwa zaidi na udanganyifu uliozagaa katika sehemu mbalimbali za nchi. Hata hivyo, Eide alisisitiza ni muhimu kwa Afghanistan kuendelea na kadhia ya kuanzisha taratibu na taasisi za kidemokrasia katika Afghanistan. Eide alikumbusha watumishi wa Shirika la UM la Kuongoza Misaada katika Afghanistan (UNAMA) walionyesha juhudi kubwa, iliohatarisha hata maisha yao, katika ukusanyaji wa ripoti zilizotakikana kutathminia upigaji kura nchini mnamo Siku ya Uchaguzi. Wakati huo huo alisema hadhi ya taarifa zilizokusanywa ilikuwa na uaminifu usio imara, uliobadilika badilika, na mara nyingi ilikuwa ni shida kuzithibitisha kihakika taarifa hizo. Licha ya yote hayo alitilia mkazo kwamba ni lazima kwa WaAfghani kuruhusiwa fursa ya kupiga kura, na kura halali zilizopigwa na umma, ambao ulikabiliwa na hata hatari ya maisha, ni lazima zihisabiwe.