Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya mwaka ya UNICEF juu ya hifadhi ya watoto imesisitiza bidii zaidi zahitajika kuwalinda watoto dhidi ya udhalilishaji

Ripoti ya mwaka ya UNICEF juu ya hifadhi ya watoto imesisitiza bidii zaidi zahitajika kuwalinda watoto dhidi ya udhalilishaji

Ripoti ya mwaka ya UNICEF kuhusu hifadhi ya watoto kimataifa imeeleza kwamba licha ya kuwa karibuni kulipatikana maendeleo kwenye suala hilo, watoto bado wanaendelea kudhalilishwa na kukabiliwa na vitendo karaha kadha wa kadha dhidi yao.

Mathalan, imethibitika ya kuwa katika baadhi ya nchi watoto wa kike huteswa na vitendo vya kutumiliwa mabavu dhidi yao, na halafu hunajisiwa kihorera bila ya wakosa kujali kuadhibiwa. Vile vile watoto wa umri mdogo kwenye sehemu mbalimbali za dunia, hutoroshwa na kujikuta ugenini wakifanya vibarua vya lazima, na kuna watoto wadogo wengine ambao hutekwa nyara na hulazimishwa kushiriki kwenye mapigano na makundi ya waasi. Madhila kama haya ni baadhi tu ya unyanyasaji na makandamizo wapatayo watoto wanaohitajia kisheria kutekelezewa haki zao halali za kimsingi. Mkuu wa Shirika la UNICEF anayehusika na Hifadhi ya Watoto, Susan Bissel, kwenye mahojiano na Idhaa ya UM alikumbusha kwamba hairidhishi kusikiliza ripoti za makandamizo ya watoto bila ya jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za vitendo zitakazosaidia kuwapatia waathirika watoto, hifadhi na ulinzi bora, kwa kulingana na sheria ya kimataifa. Alisema kunahitajika kukusanywa takwimu hakika zitakazobainisha uovu wa udhalilishaji wa watoto, kama zile takwimu zilizokusanywa karibuni na UNICEF, takwimu zenye uwezo wa kuhamaisisha wenye mamlaka kwenye Mataifa Wanachama, kuchukua hatua za dharura za kuwapatia watoto ulinzi bora, dhidi ya madhila yanayosumbua maisha yao:

""Kuwa na takwimu hakika humwezesha mgombania haki za mtoto, kutetea vizuri zaidi juu ya haja kuu ya kuwapatia watoto ulinzi unaofaa na hifadhi bora dhidi ya mateso. Ikiwa unazungumzia visa tu, na hadithi za masaibu wanayopata watoto kama riwaya, itakuwa ni vigumu kuhamasisha serikali za kimataifa na wenye madaraka kukamilisha kwa vitendo, na kufadhilia fedha zinazohitajika kukabiliana na tatizo hilo pamoja na huduma nyengine ziada za kusaidia ustawi wa watoto."

Ripoti ya UNICEF ilieleza kwamba kwa mara ya kwanza katika shughuli zake, ilifanikiwa kukusanya takwimu zinazoaminika kuhusu masuala kadha yenye kuathiri watoto, ikijumlisha masuala ya ukandamizaji wa kijinsiya na takwimu juu ya watoto wanaotoroshwa kuendeleza vibarua vya lazima nje ya nchi zao, pamoja na matatizo yanayohusu ndoa za umri mdogo, na adhabu za kimwili wapatazo watoto. Kwa mfano, hivi sasa watoto milioni moja duniani wanakadiriwa kuwa wamewekwa vizuizini na kwenye magereza, kwa mujibu wa mujibu wa takwimu zilizokusanywa kutoka nchi wanachama 44. Kadhalika, watoto wadogo milioni 150 baina ya umri wa miaka mitano mpaka 14, wamekutikana kushirikishwa kufanya kazi za lazima katika sehemu mbalimbali za dunia. Bissel alieleza, kama ifuatavyo, kwamba UNICEF, kwa kushirikiana na serikali za kimataifa pamoja na wadau wengine husika, walifanikiwa kwenye juhudi zao kupunguza ajira ya watoto wa umri mdogo na kukomesha ile tabia inayokiuka haki za mtoto ambapo watoto wa kike, wa umri mdogo, hulazimishwa kuolewa:

"Kuna nchi nyingi ulimwenguni ambapo umri wa ndoa ni mdogo sana, na tunatambua dhahiri ya kuwa ndoa za watoto wa umri mdogo, kusema kweli, hutengua haki za kimataifa za mtoto, na mtoto wa kike anayeolewa angali na umri mdogo, hasa akishika mimba, afya yake huwa hatarini. Sote tunaelewa kwamba watoto wa kike wanaojifungua kabla ya kutimia miaka 15 wana hatari ya kufariki, mara tano zaidi, wakati wa uzazi kushinda wanawake waja wazito wa umri ya miaka ya ishirini."

Lakini juu ya matatizo yote hayo, Ripoti ya UNICEF ilibainisha vile vile mafanikio yaliopatikana kwenye maendeleo ya watoto, kwa mfano, ilieleza juu ya ongezeko kubwa la idadi ya watoto wanaosajiliwa baada ya kuzaliwa, kadhia inayowapatia watoto hawo vyeti vya kuzaliwa vinavyowawezesha kupata elimu na huduma nyenginezo za kimsingi. Kadhalika, Ripoti ya UNICEF imethibitisha kupungua kwa kiwango kikubwa ulimwenguni, ile tabia yenye madhara ya kutahiri watoto wa kike, katika nchi 29 zinazoendeleza utamaduni huo wa kikale, uliopitwa na wakati.