Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ijumamosi ya tarehe 10 Oktoba (2009) huadhimishwa na UM kuwa ni Siku ya Kuwakumbuka Wagonjwa wa Akili Duniani. Risala ya KM kuihishimu siku hii ilieleza siku hii huupatia umma wa kimataifa fursa ya kuhamasisha walimwengu kuchangisha fedha na misaada mengine muhimu inayohitajika kukamilisha malengo ya kutoa uangalizi bora na uuguzaji unaoridhisha wa maradhi ya akili kwa wagonjwa husika, hasa katika mataifa yanayoendelea ambapo mahitaji ya huduma hiyo ni makubwa na uwezo uliopo kukabili janga hilo ni haba sana.

Ijumaa KM Ban Ki-moon alishtumu vikali shambulio liliotendeka kwenye marikiti ya mji wa Peshawar, Pakistan ambapo watu 49 waliripotiwa kuuawa, ikijumlisha watoto na wanawake, na watu kadha wengineo kujeruhiwa. KM alisema hakuna kisingizio cha aina yoyote wala mapambano ya kuishi yenye kuhalalisha utumiaji wa mabavu wa kihorera na vurugu kama lile liliotukia kwenye soko la Peshawar. KM amezitumia aila za waathirika wa shambulio pamoja na Serikali ya Pakistan, mkono wa pole na kuwaombea majeruhi wote wapone haraka.

Ofisi ya UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) imeripoti hali ya usalama Yemen kaskazini bado ni mbaya, ni ya wasiwasi na yenye kigeugeu kikubwa, na wenye kuumia na kusumbuliwa zaidi kimaisha na mgogoro huo, UNHCR iliongeza kusema, huwa nia raia wa kawaida. John Holmes, Naibu KM wa UM anayehusika na masuala ya kiutu, mnamo siku ya Ijumaa alizuru kambi moja ya Yemen kaskazini ambapo kuna makazi ya muda kwa wahamiaji wa ndani ya nchi 6,000 walioathirika na mapigano baina ya vikosi vya Serikali na kundi la Al Houthi, na ambao hufadiliwa misaada ya kihali na mashirika ya UM. Tawi la Yemen la Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) limearifu familia 30 zilizong'olewa mastakimu, kwa sababu ya mapigano, katika mji wa kaskazini-magharibi wa Haradh, huwasili kila siku kwenye eneo la makazi ya muda kutafuta hifadhi na huduma za kimsingi. Baadhi ya wahamiaji hawa OCHA ilisema walitembea kwa miguu karibu siku tano, kwa kupitia sehemu za milimani ili kuepuka mapigano, na wanapofika kambi za wahamiaji huwa taabani sana na hoi kabisa na huhitajia kupatiwa misaada ya kihali kunusuru maisha yao. OCHA inasema maeneo wanapoelekea wahamiaji kuomba hifadhi, mara nyingi huwa hayana huduma za kimsingi, kama maji safi na salama, na ilivyokuwa asilimia kubwa ya umma huu umekosa uwezo wa kumudu maisha, kwa hivyo hutegemea kufadhiliwa misaada ya kihali kutoka wahisani wa kimataifa. Takwimu za OCHA zimeeleza kuwa tangu mapigano kufumka tena katika siku za ya karibuni Yemen kaskazini idadi ya wahamiaji wa ndani ya nchi imefura na imeshafikia wahamiaji 150,000 hivi sasa.

Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu, John Holmes Ijumatatu ataelekea Philippines kwa ziara ya siku mbili, kutathminia mahitaji ya dharura huko baada ya Dhoruba ya Ketsana na Tofani Parma kugharikisha sehemu kadha za nchi mnamo siku za karibuni. Holmes atakapokuwepo Philppines atakutana kwa mashauriano na viongozi wa Serikali, ikijumlisha Raisi Gloria Macapagal Arroyo, wajumbe wa Baraza la Mawaziri, ikijumlisha Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Kuratibu Misaada ya Maafa, Waziri wa Ulinzi, na pia atakutana na watumishi wakaazi wa UM, wajumbe wa Timu ya UM ya Kuratibu na Kutathminia Maafa (UNDAC) na wale wafadhili wa kimataifa kuchanganua mahitaji hakika kwa maeneo yalioathirika na dhoruba za matofani. Ripoti za UM zinaeleza hali mbaya imetanda katika eneo la Luzon kaskazini, ambapo mvua zisiokwisha zinaendelea kunyesha na kuzidisha mafuriko na kuongeza idadi ya watu wanaohitajia kusaidiwa kidharura na maafa hayo.

Ofisi ya OCHA imeripoti karibuni kuanzishwa na jumuiya ya kimataifa kampeni ya kuchangisha dola milioni 38, kusaidia juhudi za Serikali ya Indonesia kumudu mahitaji ya dharura ya jamii za Sumatra Magharibi, umma ambao ulidhurika na tetemeko la ardhi liliopiga eneo lao hivi majuzi. Msaada wa Dharura wa UM utatumiwa katika miezi mitatu ijayo kuhudumia zile sehemu zilizoathirika sana na maafa, ikijumuisha miji ya Padang na Pariaman. Mashirika 11 ya UM, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na mashirika mengine 18 yasio ya kiserikali, yameomba yafadhiliwe msaada wa dharura na wahisani wa kimataifa kuwawezesha kuhudumia miradi ya kiutu 74 iliokusudiwa kukidhi mahitaji ya waathirika wa maafa katika Indonesia.

Ijumaa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu imetangaza kukaribisha, kwa ridhaa, uamuzi wa Serikali ya Iraq, wa kuwaachia huru wanachama 36 wa Shirika la Mujahedeen la Umma wa Iran, ambao walitiwa ndani na vikosi vya usalama vya Iraq kuanzia mwisho wa mwezi Julai baada ya makazi yao kwenye Kambi ya Wahamiaji ya Ashraf ilipovamiwa, na kudhibitiwa kimabavu na askari wa usalama. Kwenye operesheni hiyo watu 11 waliripotiwa kuuawa na darzeni kadha wengine walijeruhiwa. Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu imekumbusha kwamba wenye mamlaka ya utawala, kwa kulingana na kanuni za kimataifa, wanawajibika kuhishimu kihakika haki za wakazi wa kambi za wahamiaji - ikijumlisha ile haki ya kutowarejesha Iran wahamiaji wa Kambi ya Ashraf kwa kukhofia watakaporejeshwa huenda wakateswa.

Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeeleza kufanikiwa kugawa msaada wa tani 22,000 za chakula kwa raia muihitaji milioni 1.3 nchini Usomali mnamo mwezi Septemba. WFP iliripoti kuwa ingelihudumia msaada ziada wa tani 48,000 za chakula mwezi uliopita, kulisha watu milioni 3 katika Usomali, pindi ingelifadhiliwa mchango maridhawa na wahisani wakimataifa kuendeleza kadhia hiyo. WFP ilisema ililazimika kuhudumia umma muhitaji Usomali kiwango haba cha misaada ya chakula kwa sababu mchango uliopokelewa ulikuwa chini ya nusu ya msaada halisi uliohitajika kuendesha operesheni zake Usomali. Kwa mujibu wa taarifa ya karibuni ya UM, Shirika la WFP linatakiwa lifadhiliwe msaada wa dharura wa dola milioni 195 utakaoliwezesha shirika kuhudumia vyema chakula Wasomali muhitaji milioni 3.3 kwa kipindi cha hivi sasa mpaka mwisho wa Aprili 2010.

Juu ya fujo na vurugu liliozuka Guinea wiki za karibuni, Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu ameripoti kuwa anazingatia namna ya kusaidia kuanzisha uchunguzi juu ya tukio hilo - na kuhakikisha ukaguzi unaaminika - kwa sababu ya kuenea nchini hali ya wasiwasi ya kisaiasa na usalama ulioregarega, kwa ujumla. Pillay anakhofia hatari iliopo na madhara yatakayotukia kwa umma wa Guinea pindi uchunguzi utaanzishwa bila ya kupokea kutoka wenye mamlaka itakayothibitisha kuwa mashahidi hawatoteswa wala kutishwa, na watapatiwa ulinzi na usalama unaoridhisha baada ya kutoa ushahidi mbele ya tume ya UM. Kadhalika Ofisi ya Kamishna wa Haki ZA Binadamu ilisema itahitajia kupewa fursa na uwezo huru wa kuzuru maeneo yote husika ya Guinea na kuendeleza uchunguzi wao kama inavyohitajia. Mafanikio ya kadhia hiyo yanategemea ushirikiano utakaopatiwa UM kutoka wenye mamlaka Guiinea, ambao karibuni walitangaza kuunda Kamisheni ya Uchunguzi yao wenyewe. Hivi sasa Pillay anakusanya taarifa juu ya matukio ya vurugu la katika Guinea, kutoka watu na taasisi mbalimbali, kwa ushirikiano na mashirika mengine ya UM; na pia anazingatia mifumo kadha ya kisheria itakayoweza kutumiwa kuendeleza uchunguzi wa kina, unaotumainiwa kufanyika nchini Guinea haraka. Wakati huo huo Ofisi ya UM juu ya Haki za Binadamu imebainisha kwamba ofisa wake mshauri wa mamsuala ya haki za binadamu yupo Guinea tangu 2008.

Wanamuziki mashuhuri wataokusanyika mjini Nairobi, Kenya mwisho wa wiki kuhudhuria tafrija ya shirika la MTV la kuzawadia Tunzo ya Muziki wa Afrika (MAMA) wanaashiriwa kusaidia pakubwa katika kuilimisha vijana juu ya hatari ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI na kuwahamasisha kubadili tabia ya kujamiana kihorera bila ya kuzingatia hifadhi kinga dhidi ya maradhi maututi haya. Michel Sidibé, Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Mradi wa Pamoja wa Mashirika ya UM Dhidi ya UKIMWI/VVU (UNAIDS) alisema taadhima hiyo itawawezesha wanamuziki mashuhuri wa Afrika "kuharakisha kuamsha hisia za kiakili na kwenye nyoyo za vijana wa Afrika" kuhusu hatari ya maambukizo ya virusi vya UKIMWI. Kwa mujibu wa ripoti za wataalamu wa UM, vijana wa kati ya umri wa miaka 14 mpaka 24 ndio wanaojumlisha idadi mpya ya watu wanaoambukizwa na virusi vya Ukimwi, na wingi wao hukosa hata taarifa kinga za kimsingi juu ya athari hatari za maradhi hayo. Takwimu zilizokusanywa katika nchi 64 juu ya tatizo la maambukizi ya VIRUSI VYA ukimwi (VVU) zimethibitisha asilimia 40 ya vijana wa kiume na asilimia 38 ya vijanawa kike wa umri husika ndio wenye maarifa ya jumla na ripoti sahihi juu ya VVU na namna ya kujikinga na maambukizi ya vijidudu hivyo.