Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM ameiarifu Baraza la Usalama kwamba ana nia ya kumteua HanyAbdel Aziz wa Misri kuwa Mjyumbe Maalumu kwa Sahara ya Magharibi na Mkuu wa Shirika la um Kusimamia Kura ya Maoni katika Sahara Magharibi (MINURSO). Abdel-Aziz atachukua mafasi ya Julian Harston, ambaye ameteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi wa Ofisi ya UM Belgrade kuanzia 01 Machi 2009. Abdel-Azizi ameshaitumikia UM kwa miaka 25, ambapo pia alitumikia mashirika manane ya UM yanayohusika na ulinzi amani na huduma za kugawa misaada ya kiutu. Hivi sasa Abdel-Aziz anatumikia ni Mkurugenzi wa Huduma za Misaada wa Shirika la MONUC katika JKK (DRC).

Hii leo kwenye mji wa Jerusalem, Naibu Mratibu wa UM juu ya Mpango wa Amani Mashariki ya Kati, yaani Robert Serry, alizuru majengo ya Msikiti wa Bait al-Mukaddas kutathminia kihakika hali ilivyo kufuatia mapambano yaliozuka huko karibuni baina ya wafuasi wa dini ya KiIslam na wale wanaofuata dini ya Kiyahudi, ikiwa miongoni mwa juhudi za kimataifa kupunguza hali hiyo ya wasiwasi. Baadaye Serry alituma ripoti ya matokeo ya ziara yake kwa Raisi wa WaFalastina, Mahmoud Abbas, Waziri Mkuu wa WaFalastina, Salam Fayyad, na mpatanishi wa Shirika la Ukombozi wa Falastina, Saeb Erekat, na vile vile Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Danny Ayalon. Kadhalika, Serry alikutana Amman na maofisa wa vyeo vya juu wa Serikaliya Jordan ambao walisailia pamoja mada ya Jerusalem. Alionya uchochezi wa aina yoyote, utakaofanywa na makundi husika kuhusu hadhi ya maeneo matukufu ya Jerusalem, ikichanganyika na vitendo vya kukasirisha vinavyofanyika katika sehemu ya Jerusalem Mashariki ni mambo ambayo hayatoleta natija zozote kuhusu hadhi ya utakatifu wa maeneo hayo au mpango wa amani ya eneo. Alisema baada ya kuzuru msikiti wa Al Aqsa ilimdhihirikia wazi yeye binafsi kwamba mvutano uliojiri kwenye majengo hayo bado unafukuta, licha ya kuwa hali ya wasiwasi kwa sasa huko imepungua kidogo. Aliongeza kwamba watu wote aliokutana nawo wanaohusika na siala la Jerusalem aliokutana nawo walimuahidi ya kuwa wangelipendelea kuona amani inarejea kwenye eneo lao.

Naibu KM juu ya Masuala ya Misaada ya Kiutu, John Holmes Alkhamisi alitarajiwa kuanza ziara ya siku tatu Yemen, ikiwa katika juhudi za kutayarisha huduma za kuwasaidia wale raia wanawake, wanaume na watoto, ambao maisha yao yalipinduliwa chini juu na mapigano ya majuzi baina ya vikosi vya Serikali na waasi wa kundi la Al-Houthi. Holmes anatazamiwa kuzuru moja ya kambi tano za makazi ya muda zilizoanzishwa kuhudumia kihali wahamiaji wa ndani ya nchi. Kadhalika Holmes atakutana na maofisa wa serikali na wahudumia misaada ya kiutu waliopo kwenye sehemu za uhasama. Mnamo tarehe 02 Septemba 2009, jumuiya ya kimataifa iliendeleza kampeni ya kuchangisha dola milioni 23.7 zinazotakikana kuhudumia kidharura shughuli za kunusuru maisha kwa waathirika raia wa mapigano. UM umearifu kwamba fedha ilizopokea kwa sasa zinajumlisha kiwango kidogo kabisa cha msaada unaotakiwa kumudu shughuli zake, msaada ambao umekamilisha asilimia 16 tu ya jumla iliyopendekezwa kuchangishwa mwezi Septemba, sawa na dola milioni 3.8 kati ya dola milioni 23.7.

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kwamba linajaribu kuendeleza uchunguzi wa kuthibitisha chanzo cha shambulio la kutumia risasi, liliotukia Ijumanne kwenye kambi ya wahamiaji ya Gihinga iliopo mpakani baina ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) na Burundi. Kwa mujibu wa taarifa za watu walioshuhudia tukio hilo, vikosi vya usalama vya Burundi vilionekana kufyatua risasi angani kwa makusudio ya kuwatawanya umati wa wahamiaji wa JKK, umma uliolalamika kunyimwa ulinzi unaofaa, umati ambao uligoma kupelekwa uhamishoni kwenye kambi nyengize za makazi ya muda mbali na eneo la mpakani. Watumishi wa UNHCR na wafanyakazi wengine wa UM hawajakuwepo kwenye eneo tukio hilo lilipojiri, lakini UNHCR iliarifiwa kwamba hakuna aliyejeruhiwa na risasi zilizopigwa angani na vikosi vya usalama vya Burundi.

Wataalamu wa sheria wanaowakilisha Idara ya UM juu ya Operesheni za Amani (DPKO) wameanza ziara ya uchunguzi ya siku 10 katika Cote d'Ivoire kuangalia namna sheria zinavyotekelezwa ndani ya nchi, na kutathminia usimamizi wa magereza na uhusiano wa kikazi wa mahakama na sekta nyenginezo za kijamii. Ijumatano wataalamu hawa wa UM walizuru sehemu za magharibi kwa mikutano na watumishi wa UM na wafanyakazi wa Serikali, ambao walishauriana kuhusu suala la kueneza wafanyakazi wanaohusika na shughuli za mahakama na magereza katika sehemu zote za nchi, kufuatia miaka kadha ya vurugu, uhasama na fujo katika Cote d'Ivoire. Kwa mujibu wa Shirika la UM Linalosimamia Huduma za Amani katika Cote d'Ivoire (ONUCI) ziara ya wataalamu wa Idara ya DPKO itaiwezesha UM na jumuiya ya kimataifa, ambayo ilihusika katika kuleta mageuzi ya kuridhisha kwenye sekta za magereza na mahakama, itasaidia kukadiria maendeleo yaliopatikana na masula yaliosalia yenye kuhitajia suluhu ya mapema nchini Cote d'Ivoire katika kuendeleza shughuli hizo.

Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limetuma timu ya ukaguzi kwenye eneo la Fizi, katika jimbo la Kivu Kusini, kundi ambayo hujumlisha makamanda wa vikosi vya UM, ambao watachunguza namna makabila ya wapiganaji wa Mai Mai yalivyounganishwa na jeshi la taifa baada ya kusalimisha silaha. Ukaguzi huu unafannyika baada ya makundi fulani yalipolalamika kuwa na shaka juu ya utaratibu wa kuwapokonya silaha, katika kipindi ambapo vikosi vya UM na askari jeshi wa taifa walipokuwa wakiendeleza operesheni kali za pamoja, dhidi ya waasi wa Kihutu wa Rwanda. Ziara ya timu ya ukaguzi imefanikiwa kuondosha mashaka walionayo kundi la Mai Mai, kundi la jeshi la mgambo ambalo kwa sasa limesharuhusu wapiganaji 450 kusalimisha silaha na kujiunga na jeshi la taifa. Wafuasi kadha wa Mai Mai vile vile sasa hivi wanapatiwa mafunzo ya kijeshi kwenye kambi zinazoendeshwa na UM.