Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya raia wa JKK wafukuzwa Angola, imeripoti OCHA

Maelfu ya raia wa JKK wafukuzwa Angola, imeripoti OCHA

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti wiki hii ya kwamba maelfu ya raia wa JKK wanaendelea kufukuzwa na kuondolewa Angola kwa sasa hivi, katika mazingira ambayo ni ya kutisha na kushtusha kabisa.

Kwa mujibu wa msemaji wa OCHA, Severine Flores, watu waliofukuzwa nchi hawajaruhusiwa hata kuchukua mali zao na walinyanganywa kila kitu. Alisema mabavu yaliripotiwa kutumiwa dhidi ya raia wa Kongo, na hata baadhi yao walinajisiwa na kunyanyaswa na kufanyiwa maonevu kadha wa kadha dhidi yao. Baadhi ya watu waliofukuzwa waliripoti kwa UM kwamba waliondoshwa Angola kimabavu na vikosi vya usalama pamoja na watu wa kawaida, ambao "waliingia kwa nguvu majumbani mwao, na kuwapiga na halafu kuwanyanganya mali zao na kukimbia nazo." Fungu kubwa la raia waliofukuzwa Angola walikimbilia mji wa Boma, katika jimbo la Bas-Kongo, katika JKK na hivi sasa wanaishi na jamaa zao. Msemaji wa OCHA alieleza ya kuwa idadi hakika ya watu walioondoshwa Angola haijathibitishwa bado na UM, lakini mashirika ya kizalendo yasio ya kiserikali yanakadiria watu 18,000 walifukuzwa Angola tangu mwezi Julai, ikiwa miongoni mwa maelfu ya Wakongomano ambao huwa wanafukuzwa Angola kila mwaka.