Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoro wa pili wa makosa ya jinai ya halaiki Rwanda ametiwa mbaroni na ICTR

Mtoro wa pili wa makosa ya jinai ya halaiki Rwanda ametiwa mbaroni na ICTR

Ofisi ya Msemaji wa KM imeripoti kukamatwa kwenye mji wa Kampala, Uganda kwa Idelphonse Nizeyimana, aliyeshtakiwa na Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR) kushiriki kwenye mauaji ya Watutsi na Wahutu wenye siasa za wastani nchini Rwanda katika 1994.

Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR) imethibitisha kutiwa mbaroni kwa Nizeyimana, kitendo ambacho kimekaribishwa na KM. Mahakama ilimshtaki mtuhumiwa, mwezi November 2000, makosa ya kushiriki kwenye "mauaji ya halaiki, kunajisi kimabavu watu na vitendo vyengine vilivyokiuka kanuni za kiutu". Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limeripoti Idelphonse Nizeyimana alikuwa kiongozi wa ngazi ya juu kwenye lile kundi la waasi la FDLR, liliokuwa likifanya fujo na kupalilia vurugu katika jimbo la Kivu Kaskazini. Kushikwa kwa mtuhumiwa huyu, iliongeza kusema ripoti ya MONUC, kunamaanisha hatua muhimu katika kudhibiti tabia ya kufanya makosa ya jinai yanayokiuka haki za binadamu bila ya kukhofu adhabu, na humaanisha mataifa ya maeneo ya Maziwa Makuu yamewania kutekeleza ahadi zao za kuimarisha usalama na amani ya maeneo yao kwa kufuata sheria.