Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR imehadharisha wahamiaji waliopo Burundi kutorudi JKK kwa sababu ya vurugu

UNHCR imehadharisha wahamiaji waliopo Burundi kutorudi JKK kwa sababu ya vurugu

Andrej Mahecic, msemaji wa shirika la UM linalohudumia wahamiaji la UNHCR, ameripoti kutoka Geneva kwamba taasisi yao imewashauri wahamiaji 2,300 wa JKK waliopo kwenye kambi ya Gihinga, katika jimbo la Mwaro, Burundi ya kati kutorejea makwao hivi sasa, kwenye lile jimbo la vurugu la Kivu Kusini, liliopo eneo la mashariki la JKK.

Kwa sababu ya kuendelea kwa operesheni za kivita Kivu Kusini, hali ya usalama kwa raia huko kwa sasa ni ya wasiwasi, ilinasihi UNHCR. Kwa mujibu wa taarifa za UM wenye mamlaka ya Serikali katika JKK, na pia UNHCR, hawana uwezo wa kuwahakikishia usalama wale wahamiaji wanaotaka kurejea makwao, wala hawana uwezo wa kuhudumia kihali wahamiaji ili waanzishe maisha mapya. UNHCR pia imeeleza kwamba mazingira ya wasiwasi bado yameselelea kwenye eneo la vurugu, hali ambayo ndio iliosababisha wahamiaji kuelekea uhamishoni Burundi katika Juni 2004, hali iliofuatiwa na mauaji ya halaiki katika Gatuma mnamo mwezi Agosti 2004. Kisheria UNHCR inaunga mkono uamuzi wa wahamiaji, binafsi, kurejea makwao, kwa khiyari, pindi hali inaruhusu, na kuhakikisha kuna utulivu na amani makwao. Lakini katika kipindi cha hivi sasa, hali katika eneo la mashariki la JKK hairuhusu kwa wahamiaji wa Kongo kurejea kutoka Burundi.